Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hasan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa filamu maarufu ya Royal Tour April 28,2022 katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa AICC jijini Arusha.
Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari Mkuu wa mkoa wa Arusha John Mongela amesema mkoa wa Arusha umepata heshima ya kuwa mwenyeji katika tukio kubwa la uzinduzi wa filamu ya Royal Tour.
Amesema Rais Samia atakuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa filamu hiyo ikiwa ni mara ya kwanza kufanyika nchini tangu ilipozinduliwa rasmi nchini Marekani Aprili 18,2022 na baadae Aprili 2,2022 katika jiji la Los Angeles nchini Marekani.
Mongela amedai kuwa kwa hapa nchini uzinduzi wa filamu hiyo yenye lengo la kuvutia watalii na wawekezaji nchini utafanyika ukumbi wa mikutano AICC kwa kuwa Arusha
ni kitovu cha utalii nchini.
Aliongeza kuwa katika uzinduzi huo wanatarajia kuwa na wageni na viongozi wa kitaifa,mabalozi, wawekezaji,wadau wa utalii na uhifadhi pamoja na wananchi kutoka mikoa ya jirani.
Alisema kwa sasa idadi ya watalii wanaotembelea imeongezeka kutoka wastani wa watalii laki 562,549 mwaka 2020 hadi watalii 788,933 kwa mwaka 2021.
Ametoa rai na kuhamasisha wananchi hasa wa mikoa ya Arusha na Kilimanjaro kujitokeza katika maeneo watakayoainisha haswa katika barabara kwa ajili ya kumpokea Rais Samia na ujumbe wake kuelekea uzinduzi wa filamu hiyo.
Social Plugin