Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

AKAMATWA NA MENO YA TEMBO, NYAMA YA TEMBO NDANI YA HIFADHI YA KATAVI


Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi Ali Makame Hamad akionesha meno mawili ya tembo mbele ya waandishi wa Habari ambayo amekamatwa nayo mtuhumiwa Mashaka Mavunje mkazi wa Kijiji cha Mtakuja Tarafa ya Nsimbo Wilaya ya Mpanda amekamatwa nayo ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Katavi. Picha na Walter Mguluchuma
Kamanda Polisi Mkoa wa Katavi Ally Makame Hamad akionesha bunduki aina ya gobore aliyokamatwa nayo mtuhumiwa Mashaka Mavunje Mkazi wa Kijiji cha Mtakuja aliyokutwa nayo akiwa na meno mawili ya tembo na nyama kilo tisini akiwa ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Katavi akifanya ujangili wa kuua wanyama

Na Walter Mguluchuma -Katavi

Jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi kwa kushirikiana na askari wa Hifadhi ya Taifa ya Katavi wamefanikiwa kumkamata Mashaka Mavunje (42) Mkazi Kijiji cha Mtakuja Tarafa ya Nsimbo Wilaya ya Mpanda akiwa na meno ya tembo mawili na nyama ya tembo kilo 90 akiwa ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Katavi .

Kwa mujibu wa Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Katavi Ali Makame Hamad mtuhumiwa huyo amekamatwa Aprili 13,2022 majira ya saa saa nane mchana katika maeneo ya Kashoka ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Katavi .

Amesema mtuhumiwa huyo alikamatwa kufuatia taarifa walizokuwa wamezipata jeshi la polisi na TANAPA za kuwa mtu huyo anajihusisha na ujangili wa kuua wanyama ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Katavi na ndipo walipoanza kufanya msako mkali wa kumsaka mtuhumiwa huyo .

Kamanda Hamad ameeleza kuwa mtuhumiwa Mashaka Mavunje siku hiyo ya tukio alikamatwa ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Katavi akiwa na meno mawili ya mnyama tembo yenye uzito wa kilogramu 3.1 na nyama ya tembo kili tisini .

Pia alikamatwa akiwa na silaha moja aina ya gobore ambayo ilitumika kwa ajiri ya kumuuwa tembo huyo pamoja na panga moja na kisu kikubwa aina ya sime .

Amebainisha kuwa mtuhumiwa huyo aliingia ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Katavi akiwa na silaha bunduki aina ya gobore ambapo alimpiga na kumuua mnyama tembo na kisha alimtoa meno yake na kisha aliweza kubeba kilo hizo tisini za mnyama huyo alizokutwa nazo.

Mtuhumiwa anaendelea kuhojiwa ili kuweza kupata washiriki wenzake na mara baada ya upelelezi kukamilika jalada litafikishwa katika ofisi ya Taifa ya mashitaka Mkoa wa Katavi kwa taratibu za kisheria .

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com