Na Doreen Aloyce, Dodoma
Jeshi la Uhamiaji Mkoa wa Dodoma linawashikilia raia watano wa Ethiopia akiwemo Mtanzania mmoja kutokana na kuingia nchini kinyume cha sheria na utaratibu wa nchi pamoja na raia mmoja wa Tanzania Tito Mbwilo mwenye umri wa miaka 43 mkazi wa Iringa na Tunduma ambaye alikuwa akisafirisha wahamiaji hao.
Akiongea na waandishi wa Habari Afisa uhamiaji Mkoa wa Dodoma Bahati Mwaifuge amesema wahamiaji hao haramu walikamatwa April 3 mwaka huu katika kijiji cha Mtera wakielekea Tunduma Mkoa wa Songwe.
"Jeshi letu la uhamiaji tumefanikiwa kuwakamata wahamiaji haramu watano akiwemo mtanzania mmoja wakisafirishwa kwenye gari yenye namba za usajiri T991 DXB Toyota Rumioni ambalo lilikuwa linaendeshwa na Tito Mbwilo akijua ni kosa",amesema Bahati.
Aidha amesema baada ya kuwatia mbaroni wahamiaji haramu hao, Dereva wao Tito Mbwilo alijaribu kutoroka bila mafanikio kutokana na umahili wa Askari ambapo waliweza kimdhibiti na kumuweka chini ya ulinzi.
Hata hivyo alitoa onyo kwa wasafirishaji wote wanaojihusisha na wahamiaji haramu katika Mkoa wa Dodoma kuacha mara moja na kwamba jeshi tayari limebaini wamebadili mbinu kutoka magari makubwa na kutumia magari madogo.
"Niwaombe wananchi wote wakiwemo wa Mtera kuendelea na ushirikiano kutoa taarifa za kusafirisha wahamiaji haramu jambo ambalo litasaidia katika utendaji kazi wetu",alisema Bahati.