Na Alex Sonna
VINARA wa Ligi Yanga wametoka nyuma na kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Azam FC Mchezo wa Ligi Kuu ya NBC uliopigwa uwanja wa Chamazi Complex nje kidogo ya jiji la Dar es salaam.
Azam FC walikuwa kwanza kuliona lango la Yanga dakika ya 10 likifungwa na Mshambuliaji Rodgers Kola akipokea pasi ya Bruce Kangwa.
Mnamo dakika ya 17 Yanga walisawazisha kupitia kwa Shaban Djuma kwa mkwaju wa Penalti baada ya golikipa wa Azam Ahmed Salula kudaka miguu ya Saido Ntibazonkiza
Yanga walipata bao la ushindi dakika ya 77 likifungwa na Fiston Mayele akimalizia krosi ya Shaban Djuma huku likiwa bao la kumi na moja kwa Mayele.
Kwa ushindi huo Yanga wameendelea kuufukuzia ubingwa wa 28 kwa kufikisha Pointi 51 wakiwa wamecheza mechi 19 huku Azam Fc wakibaki na Pointi zao 28 nafasi ya tatu.
Mchezo mwingine umepigwa uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza na Biashara United imeibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mbeya Kwanza.
Ligi Kuu itaendelea kesho kwa mechi moja wekundu wa Msimbazi Simba watakuwa ugenini kucheza na Coastal Union uwanja wa Mkwakwani Tanga
Social Plugin