Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

KINANA ASHINDA KWA ASILIMIA 100 UMAKAMU MWENYEKITI CCM..ATOA UJUMBE MZITO


Makamu Mwenyekiti wa chama cha Mapinduzi Abdulrahman Kinana,akizungumza baada ya kutangazwa kuwa makamu mwenyekiti.
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akipiga kura kwa ajili ya kumchagua Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM kwa upande wa Tanzania Bara Abdulrahman Kinana katika Mkutano Mkuu wa dharura uliofanyika katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma leo tarehe 01 Aprili, 2022.

…………………………………………………….

Na Alex Sonna-DODOMA

Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) wamemchagua kwa asilimia 100 aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama hicho, Abdulrahman Kinana kuwa Makamu Mwenyekiti wa chama hicho baada ya kupata kura zote za ndio 1875 zilizopigwa.

Akizungumza baada ya kushinda Abdulrahman Kinana alimshukuru Mwenyekiti wa Chama hicho Mhe. Samia Suluhu Hassan

“Juzi uliniita nikawa najiuliza nimeitiwa nini, nikajua ni katika kusalimiana.Rais akaniambia nataka uwe Makamu Mwenyekiti, nikamwambia sina hiari, sina budi kukubali, napenda kukuhakikishia Mwenyekiti nitajitahidi kadri ya uwezo wangu kufikia matarajio yako, Niseme sitokuangusha”

Kinana ameishukuru Kamati Kuu kwa kupitisha jina lake, pamoja na wajumbe wa Halmashauri kuu kwa kupitisha na kuidhinisha jina lake

“Mmenipa imani kubwa, na mimi nitakitumikia Chama changu, wana CCM na Watanzania”

Pia amemshukuru Mzee Mangula ambapo amesema kuwa amejifunza mengi kutoka kwake na kumpongeza kwa kustafu kwa Heshima

“Kama Mangula asingeamua kustaafu, basi leo nisingekuwa Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi”

Makamu Mwenyekiti Kinana aliwashukuru Wenyekiti wote kuanzia Baba wa Taifa mpaka sasa Rais Samia Suluhu Hassan na kusema kuwa mengine ni mapungufu yake mwenyewe

Aidha ameahidi kwenda kusimamia Chama kuwa imara Kidemokrasia na kusimamia haki ya kuchaguliwa bila upendeleo

“Lazima wanachama wawe Huru kutoa mawazo, hakuna mwenye hakimiliki ya mawazo, lazima tumsikilize kila mwananchi, na wanachama wakimchagua mtu kwani sisi ni nani wa kupinga”

Alisisitiza kusimamia Demokrasia na kusema ni lazima kusimamia haki

“Nimekuwa nikimsikia Rais akisisitiza mara zote katika kusimamia haki, nilimsikia akisema Vyeti peke yake siyo sifa, Vyeti viende na uadilifu, kukubalika, Nchi hii inajulikana kwa Haki ndani na nje ya Nchi”

Alisema jukumu lake la Tatu ni kwamba CCM si mali ya Serikali ila Serikali zinatokana na CCM ambapo alieleza kuwa CCM haipokei maelekezo kutoka Serikalini

“CCM haiagizwi na Serikali, CCM Inaagiza Serikali, na wanaokwenda kuomba kura ni CCM sio Serikali, niwasihi Viongozi wetu msitudhulumu hiyo haki”

Alisema Serikali inapokuwa na mapungufu wenye jukumu la kuzisemea kasoro ni Chama

“Na hatutazisemea kwa kukejeli, tutaitana kwenye Vikao vyetu vya Ndani, si sawa kwa Mwana CCM kwenda hadharani kuisema vibaya Serikali yake”

Kinana alisisitiza, Chama cha Mapinduzi ni kikubwa na kinakubalika hivyo ni lazima CCM ibaki kuwa masikio kwa Wananchi

Aliahidi utumishi uliotukuka ili Chama kuendelea kuwa imara na umoja

“Hili nalo ni la umhimu, nataka niwasishi hakuna chama cha mtu, kuna Chama cha Mapinduzi.ndani ya hiki chama hakuna ukanda, haya mambo ya ukanda, ukabila, udini tukae nayo mbali.mtu akikosa hoja, maarifa anaingia kwenye kichaka cha udini, ukabila, ubara na visiwani.hiyo si sawa kwa chama hiki, tunaweza kutofautiana kwa sababu nyingi lakini siyo kikanda au kikabila”

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com