NIT MABINGWA BONANZA LA DIWANI WA MABIBO


TIMU ya Mpira wa Miguu ya Chuo Cha Taifa Cha Usafirishaji (NIT)imeibuka mabingwa katika Bonanza maalumu lililoandaliwa na Diwani wa Kata ya Mabibo Jijini Dar es salaam baada ya kuifunga timu ya Azimio kwa magoli 3-0.

Bonanza hilo lililofanyika katika viwanja vya Shule ya Sekondari ya Loyola, mbali na mchezo wa mpira wa miguu ambao ulizishirikisha jumla ya timu 11, lilikuwa na michezo mingine ikiwemo mpira wa pete kwa wanawake, kukimbia, kuvuta kamba pamoja kufukuza kuku.

Kutokana na ushindi huo, timu hiyo ya N.I.T ilizawadiwa kikombe, seti moja ya jezi pamoja na mpira mmoja huku timu ya Azimio ambayo ndiyo imeshika nafasi ya pili ikizawadiwa seti moja ya jezi na mpira mmoja.


Akizungumza wakati wa bonanza hilo lililohudhuriwa pia na uongozi wa taasisi ya 'African Youth Empowerment' (AYE) inayojisghulisha na utafutaji wa vijana wenye vipaji vya mpira, Diwani wa Kata ya Mabibo Joseph Klerruu alisema lengo lake ni kujenga umoja miongoni mwa wanajamii wa kata hiyo.

"Tumekutana hapa kwa nia moja ya kujenga ujamaa miongoni mwetu na kufahamiana, michezo ni undugu, urafiki hivyo naamini kupitia jumuiko hili la pamoja tunazidi kuukuza undugu wetu", alisema Klerruu


Alisema pamoja na hilo, kufanyika kwa bonanza hilo limesaidia kujenga umoja na mshikamano miongoni wananchi wa kata hiyo ya Mabibo na majirani zao huku akisisitiza umuhimu wa wananchi kujiandaa na Sensa ya Watu na Makazi inayotarajiwa kufanyika Agosti 23 mwaka huu.

Alisema kuna umuhimu mkubwa wa wananchi kujitokeza na kushiriki katika sensa hiyo ili kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan katika jitihada anazozifanya kuliletea maendeleo Taifa hili.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post