SERIKALI YAELEZA UTEKELEZAJI WA MAENDELEO YA TEHAMA KATIKA KUPIMA UTENDAJI KAZI

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu) Mhe. Joyce Ndalichako (Kulia) na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama (Kushoto) wakiwa katika Mkutano na Viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi kuhusu mtazamo wa serikali ya Awamu ya sita katika Uimarishaji wa Utumishi wa Umma unaowajibika kwa hiari na Matumizi ya mifumo ya TEHAMA katika utendaji na utoaji Huduma bora katika Utumishi wa Umma,tarehe 9 Aprili, 2022 Jijini Dodoma.

Na Dotto Kwilasa Malunde 1 blog-DODOMA

WAZIRI wa Nchi,Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Jenista Mhagama amekutana na viongozi wa vyama vya wafanyakazi nchini ili kutambulisha mfumo mpya wa Usimamizi wa Utendaji kazi kwa Watumishi wa Umma (PEPMIS) kabla ya kuanza kutumika Julai Mosi mwaka huu baada ya mfumo wa awali (OPRAS) kushindwa.

Akiongea leo tarehe 9 Aprili, 2022 Jijini Dodoma, wakati wa mkutano na Viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi kuhusu mtazamo wa serikali ya Awamu ya sita katika Uimarishaji wa Utumishi wa Umma unaowajibika kwa hiari na Matumizi ya mifumo ya TEHAMA amesema Mfumo wa awali wa OPRAS uligubikwa na malalamiko mengi kwa kuwa ulikuwa hautendi haki kwa watumishi katika kupatiwa stahiki na masuala mbalimbali ikiwemo hatua zinazochukuliwa kwa mtumishi pale anapokuwa amekiuka maadili ya utumishi.

Amesema serikali inatarajia kuanza kutumia mfumo huo mpya wa kielektroniki kwa ajili ya kufanya tathimini ya hali ya watumishi wa umma kwa uwazi ili kuondokana na changamoto zilizokuwepo katika mfumo wa awali ifikapo Julai Mosi mwaka huu.


“Kuanza kutumika kwa mfumo huo ni utekelezaji wa agizo la Rais, Samia Suluhu Hassani alilolitoa kwa ofisi hiyo ili kuondoa changamoto za usimamizi wa utendaji kazi zilizojitokeza katika utekelezaji wa mfumo wa awali wa OPRAS, ambao haukuakisi hali halisi ya utendajikazi wa watumishi hali iliyoleta hisia za kupendeleana au kuoneana na kutokutumika kwa matokeo ya utendajikazi katika kufanya maamuzi ya kiutumishi,amesema.

Amesema mfumo huo mpya wa PEPMIS utakuwa ni wa kielektroniki na utaondokana na matumizi ya makaratasi  huku akiwataka  Wafanyakazi wa Vyama vya Wafanyakazi kuendelea kuwa daraja kati ya waajiri na Wafanyakazi kwa kuchochea na kuhimiza utamaduni kwa Wafanyakazi kudai haki na kutimiza wajibu wao kupitia TEHAMA.

"Ofisi hii imetekeleza maagizo ya Mhe. Rais kwa kujenga na kufanya maboresho katika mifumo ya Usimamizi wa Utendaji Kazi kwa Watumishi wa Umma (PEPMIS), Usimamizi wa Utendaji kazi katika ngazi ya Taasisi (PIPMIS),"amesema.

Vyama alivyokutana navyo Waziri huyo  ni pamoja na Wenyeviti na Makatibu wa Chama cha Wafanyakazi wa Vwanda, Biashara,Taasisi za Fedha, huduma na Ushauri(TUICO),Chama cha Wafanyakazi, Wanataaluma na Watafiti( RAAWU), Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya(TUGHE), Chama cha Wafanyakazi wa Sekta ya Huduma ya Mtandao(TEWUTA)

Vingine ni Chama cha Wafakazi wa Migodi na Kazi nyinginezo(TAMICO), Chama cha Wafanyakazi wa Mawasiliano na Uchukuzi(COTWU)(T), Chama Cha Wafanyanyakazi wa Maroli Tanzania(DOWUTA).

Jenista amevitaja vingine kuwa ni Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Nchini(TUCTA), Chama cha Wafanyakazi wa Majumbani(CHODAWU), Chama Cha Walimu Tanzania(CWT), Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa(TALGWU),Chama Cha Wafanyakazi wa Reli Tanzania(TRAWU) na Chama cha Mabaharia(TASU).

Kutokana na hayo Katibu wa Chama Cha Walimu Tanzania(CWT), Deus Seif, amesema wanaishukuru serikali kwa kuja na mfumo huo mpya ambao utasaidia kwa kiasi kikubwa kumaliza changamoto kwa watumishi wa umma.

“Mfumo wa awali wa OPRAS uligubikwa na malalamiko mengi kwa kuwa ulikuwa hautendi haki kwa watumishi katika kupatiwa stahiki na masuala mbalimbali ikiwemo hatua zinazochukuliwa kwa mtumishi pale anapokuwa amekiuka maadili ya utumishi,”amesema.

Naye, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu) Joyce Ndalichako amesema pamoja na juhudi za serikali za kupima utendaji kazi serikalini Mhe. Rais amelekeza ushirikishwaji wa Vyama vya Wafanyakazi amewataka Viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi kuendelea kuwa daraja kati ya waajiri na Wafanyakazi kwa kuchochea na kuhimiza utamaduni kwa Wafanyakazi kudai haki na kutimiza wajibu wao.


Prof. Ndalichako amesema Ofisi ya hiyo imeendelea kutekeleza maagizo ya Mhe, Rais kwa kukamilisha Mfumo wa Kielektroniki wa utoaji wa Vibali vya Kazi kwa raia wa kigeni. Mfumo huo umepunguza muda wa kushughulikia maombi ya vibali vya kazi kutoka siku za kazi 14 hadi siku 7.

 Aidha, Mfumo huo umeimarisha uwazi na uwajibikaji.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post