Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bw, Khamis Mgeja amekipongeza Chama Cha Mapinduzi chini ya Mwenyekiti wake na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kusajili timu ya ushindi kwa CCM katika chaguzi zijazo na hasa kumsajili kocha mchezaji na bingwa wa kimkakati ya ushindi Comred Abdulrahman Kinana.
Khamis Mgeja ambaye ni mwanasiasa mkongwe nchini na ambaye amewahi kuwa Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Shinyanga na mjumbe wa halmashauri kuu ya CCM Taifa aliyasema hayo alipoulizwa na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Kahama ili aelezee kuchaguliwa kwa Makamu Mwenyekiti Comred Kinana CCM itarajie nini kiuongozi kutoka kwa Kinana.
Mgeja amevipongeza vikao vyote vya chama (Kamati Kuu, Halmashauri Kuu, Mkutano Mkuu chini ya mwenyekiti Mhe. Samia Suluhu Hassan, kwa kupendekeza na hatimaye kumchagua kwa kura zote na kushinda asilimia 100% akisema hii imedhihirisha kuwa ni jinsi gani Kinana anavyokubalika kwa wana CCM na wanaimani na matarajio makubwa ya kiuongozi kutoka kwake.
Mgeja amesema CCM kumpata makamu wa aina ya Kinana ni adhimu sana CCM imefanya usajili mzuri sana sawa na kulamba dume. Sisi makada hivi sasa tunaona upele umepata mkunaji ndani ya CCM, kwani Kinana ni mchapakazi hodari na ni bingwa wa mikakati ya ushindi lakini kubwa amelelewa ndani ya chama na amekulia ndani ya chama pia amekitumikia chama kwa muda mrefu sana pamoja na nyanja mbalimbali za utumishi serikalini.
Mgeja amesema anafurahi na kufarijika yale aliyosema siku za nyuma hatimaye yametimia kuwa Chama Cha Mapinduzi na vyama vingine duniani vinavyofuata misingi za siasa za kijamaa na kujitegemea vinao mifumo yake rasmi ya kupata viongozi wazuri walioandalika ambapo alisisitiza "Mkiacha mfumo wa kupata viongozi walioandalika dhambi yake lazima iwatafune waliokuwemo na wasiokuwemo na chama lazima kitikisike".
Mgeja alimpongeza mwenyekiti wa CCM na kumuombea Mungu ambariki sana Mhe. Samia Suluhu Hassan kukirudisha chama katika mfumo wake wa asili wa kupata viongozi walioandalika na chama.
"Hata hivi sasa sekretarieti ya CCM chini ya Comred Chongolo Katibu mkuu nao wote wameandalika na chama kiuongozi na makuzi ndiyo maana mambo yanaenda vizuri na CCM inaendelea kung’ara siku hadi siku",amesema Mgeja.
Mgeja ametoa masikitiko yake na kusema ni ukweli usiopingika huko nyuma CCM iliacha njia kidogo na ilipata viongozi ambao hawajaandalika ki uongozi wa chama na hawakujulikana walikotoka hasa baadhi ya watendaji wakuu wa chama na baadhi ya viongozi na mpaka ikafika wakaja na kauli mbiu ya CCM mpya.
"Cha kushangaza sijui ile CCM ya zamani waliizika lini na wapi kumbe wakasau CCM iliyopo na waliyoikuta ni ile ile na itaendelea kuwa ile ile, ile kauli ya CCM mpya ilikuwa ni kauli ya ubaguzi mkubwa kwa wanachama ndani ya chama na kugawa matabaka ya kuonekana walio bora na wasiofaa, lakini wakasahau wanachama ndani ya CCM wote wanategemeana",ameeleza Mgeja.
Mgeja amemwelezea Comred Kinana na amejifunza mengi kutoka kwake kuwa ni kiongozi mzalendo, shupavu, mkweli, mpenda haki, aliyeshiba dini anachukia dhuruma, mnyenyekevu kwa mkubwa na mdogo, si mbaguzi wa dini, ukabila, jinsia na ukanda, mpenda mijadala ya uhuru wa mawazo na kusema. Pia na anahofu ya mwenyezi Mungu.
Mgeja amewaomba wana CCM kuyafanyia kazi maneno mazito yenye afya ndani ya chama aliyoyasema Makamu Mwenyekiti wa CCM Comred Kinana wakati anashukuru kwa wajumbe wa mkutano mkuu wa CCM Taifa kwa kumchagua.
"Mimi binafsi kama kada wa chama naomba wanachama na viongozi tubadilike tusimamie yale tuliyoaswa na makamu wetu wa CCM ili chama kiendelee kuwa imara ni lazima tusimamie haswa masuala ya Demokrasia ndani ya chama na kusimamia haki na tutambue kila mwanachama ana haki ya kuchagua na kuchaguliwa bila upendeleo, mizengwe, rushwa au umaarufu wa mwanachama na tuwe tayari kumsikiliza mwanachama hata kama uamuzi hauupendi, Naomba tuyafanyie kazi maneno ya Kinana yana maslahi makubwa ndani ya chama", alisema Mgeja.
Social Plugin