Mkuu wa Wilaya ya Bariadi Lupakisyo Kapange akiongea kwenye maadhimisho ya siku ya Muungano yaliyofanyika kiwilaya katika kata ya Nyangokolwa mjini Bariadi.
Na Costantine Mathias, Bariadi.
MKUU wa Wilaya ya Bariadi Mkoani Simiyu Lupakisyo Kapange amesema Muungano wa Tanganyika na Zanzibar utaendelea kudumu milele kutokana na viongozi na serikali zake hupatikana kwa kuchaguliwa kwa kupiga kura.
Kapange amesema Muungano umeendelea kudumu kwa sababu ya kubadilisha uongozi kwa haki na demokrasia na kwamba wamekuwa wakipokezana vijiti kwa serikali zote mbili za Tanganyika na Zanzibar.
Mkuu huyo wa wilaya aliyasema hayo jana (Aprili 26, 2022) kwenye maadhimisho ya sherehe za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambapo maadhimisho hayo yalifanyika kwa ngazi ya wilaya katika kata ya Nyangokolwa.
Kapange alisema kupitia Muungano huo wananchi wanapokea maendeleo na uimara wake umezaa maendeleo katika wilaya ya Bariadi na mkoa wa Simiyu ambapo miradi mbalimbali ya kimaendeleo inatengenezwa.
‘’Nawaomba viongozi na watendaji wenzangu twende kuwatumikia wananchi ili kuondoa kero mbalimbali zinazolikabili taifa hili… Rais Samia ameleta fedha nyingi za miradi ya maji, umeme, barabara elimu na afya, huyo ndio Rais anayelinda muungano’’ ,alisema Kapange.
Alisema serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia na watendaji wake iko imara na kwamba Rais Samia ni jasiri na anajua uchungu wa Taifa la Tanzania na wajibu wa viongozi ni kupokea, kusimamia na kutekeleza miradi ya maendeleo.
Katika hatua nyingine Kapange alisema mahitaji ya watu wa Bariadi siyo Katiba mpya na badala yake wanahitaji hospitali, umeme, madarasa, maji, barabara zinazopitika muda wote na wamechoka kuchangishwa michango.
Awali Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Bariadi Khalid Mbwana alisema katika miaka 58 ya Muungano, Halmashauri ya wilaya hiyo imenufaika na fedha nyingi za miundombinu.
"Ndani ya mwaka mmoja wa Rais Samia tumepokea bilioni 11 kwa ajili ya utekelezaji wa miundombinu ya maendeleo katika sekta mbalimbali, tumepata fedha kwa ajili ya vituo vya afya viwili vya Matongo na Miswaki na kila kimoja kinajengwa kwa milioni 500’’, alisema Mbwana.
Awali akitoa historia ya Muungano, Mwalimu Mafuru Mafuru kutoka Bariadi Sekondari alisema Muungano ni Tunu ya Taifa inayolenga kudumisha Amani, Umoja, Mshikamano na Undugu.
Mafuru aliwataka wananchi kuendelea kudumisha na kuulinda Muungano ambayo umeleta udugu na mshikamano baina ya watanzania ambao wanaishi kama ndugu licha ya kuwa na makabila tofauti tofauti.
Mkuu wa Wilaya ya Bariadi Lupakisyo Kapange akiongea kwenye maadhimisho ya siku ya Muungano yaliyofanyika kiwilaya katika kata ya Nyangokolwa mjini Bariadi.
Mkuu wa wilaya ya Bariadi Lupakisyo Kapange (kushoto) akiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Bariadi Khalid Mbwana kwenye maadhimisho ya siku ya Muungano yaliyofanyika kiwilaya katika kata ya Nyangokoliwa mjini Bariadi.
Mkuu wa wilaya ya Bariadi Lupakisyo Kapange akisaini kitabu wakati wa maadhimisho ya siku ya Muungano.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashuri ya Mji wa Bariadi Adrian Jungu (kulia) akitoa maelezo mbele ya Mkuu wa wilaya ya Bariadi Lupakisyo Kapange namna wanavyotekeleza miradi ya Maendeleo, wakati wa maadhimisho ya siku ya Muungano iliyofanyika April 26, 2022 katika kata ya Nyangokolwa mjini Bariadi.
Wananchi wakifuatilia maadhimisho ya siku ya Muungano