Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan
**
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewataka viongozi na watumishi wa umma kuwa na heshima ya kweli kutoka ndani ya mioyo yao na kila mtu kutimiza majukumu yake kwa maadili na weledi mkubwa kwa maslahi mapana ya taifa.
Rais Samia ameyasema hayo leo jijini Dodoma wakati akiwaapisha viongozi mbalimbali walioteuliwa hivi karibuni ikiwa pamoja na mawaziri waliobadilishwa kutoka wizara moja kwenda nyingine.
Katika hotuba yake Rais Samia ameabainisha kuwa licha ya serikali ya awamu ya tano kusifiwa kwa kukuza heshima kwa watumishi wa umma, lakini heshima hiyo ilikuwa ya woga, na hivyo akawataka watumishi kuwa na nidhamu kutoka ndani ya mioyo yao.
“Tunasifiwa kuwa awamu ya tano tulikuza heshima kwa watumishi wa umma, heshima iliyokuzwa ni heshima ya woga kwa sababu alikuwepo simba wa Yuda, ambaye ukimgusa sharubu anakurarua, heshima inayotakiwa iwe ya moyoni” ,amesema Rais Samia Suluhu Hassan
Aidha Rais Samia akasisitiza kuwa ataendelea kufanya kazi kwa kalamu, na kamwe hawezi kuwafokea watendaji walio chini.
Chanzo - EATV