Tionge Ziba (21), anasoma mwaka wa kwanza kwenye chuo kikuu cha Yugra State University
****
WIZARA ya mambo ya nje ya Zambia, imethibitisha kuwa mwanafunzi wa Zambia anayesoma nchini Urusi amekamatwa Jumapili iliyopita kwa kucheza muziki kwenye makaburi ya kumbukumbu ya vita ya pili ya dunia yaliyopo kwenye mji wa Khanty-Mansiysk.
Mwanafunzi huyo, Tionge Ziba (21), anasoma mwaka wa kwanza kwenye chuo kikuu cha Yugra State University kilichopo kwenye mji huo.
Kwa mujibu wa Wizara hiyo, Ziba ameachiwa kwa dhamana lakini mashtaka dhidi yake yamekidhi vigezo vya kufikishwa kwa mwendesha mashtaka wa mji huo.
Taarifa za mashtaka yake zinasema kuwa video ya msichana huyo akicheza muziki kwenye makaburi hayo ilirekodiwa mnamo Aprili 14.
Mwanafunzi huyo anadaiwa kuishirikisha video hiyo kwenye ukurasa wake wa instagram na kuandika maelezo ya video yakisema “nikitingisha…..kwa ajili ya marehemu [hawa], hakika wanalala unono usiku wa leo” maelezo ambayo kwa mujibu wa nyaraka za mahakama ni “maelezo ya kuudhi wanayodhaniwa yanadhihaki sera ya Nazi”.
Idara ya upelelezi ya jiji hilo tayari imeachia video ya Ziba akiomba radhi kwa kitendo hicho ingawa wakati video hiyo ilipokuwa inawekwa mtandaoni haikuwa imemtaja kwa jina wala utaifa wake.
Kwa mujibu wa wizara ya mambo ya nje ya Zambia shauri dhidi ya Ziba litachunguzwa kwa miezi mitatu na linatarajiwa kutoingiliana na ratiba zake za masomo.
Gazeti binafsi la Kommersant la nchini humo limesema huenda Ziba akakabiliwa na hukumu ya kulipa fidia ya kati ya $25,000 na $65,000 (TZS 60m – TZS 150m) au kufanya kazi ngumu kwa kipindi cha kati ya mwaka mmoja hadi mitano huku kukiwa na uwezekano wa kifungo cha gerezani cha hadi miaka mitano.