Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SHIRIKA LA KIVULINI LASHIRIKI KONGAMANO LA BAKWATA..LASHAURI MBINU ITAKAYOSAIDIA KUWAONDOA WATOTO MITAANI


Shirika la kutetea haki za watoto na wanawake KIVULINI limeshauri kuwa jitihada za kuwaondoa watoto wanaoishi mitaani zitafanikiwa ikiwa Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali itahakikisha kila mtoto analelewa na wazazi ama walezi wake.

Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo, Yassin Ally ametoa ushauri huo Aprili 09, 2022 wakati akizungumza kwenye kongamano la malezi bora, tabia njema na misingi ya ndoa lililoandaliwa na Baraza Kuu la Waislamu BAKWATA Mkoa Mwanza.

Amesema watoto wote waliokimbilia mitaani wana wazazi ama walezi wao lakini changamoto iliyopo hawatimizi wajibu wao wakidhani jukumu hilo ni la Serikali ama wadau wa maendeleo na hivyo kushauri Serikali kuja na mbinu za kuwadhibiti wazazi na walezi wasiowajibika kwa watoto wao.

Ally pia ameonya kuwa changamoto ya ukosefu wa malezi bora kwenye ndoa nyingi imekuwa chanzo kikubwa cha watoto kukosa maadili na kukimbilia mitaani hatua ambayo inawanyima haki zao za msingi ikiwemo kupata elimu huku wakiwa katika hatari ya kuingia kwenye vitendo hatarishi.


Naye Sheikh Mkuu wa BAKWATA Mkoa Mwanza, Sheikh Hassan Kabeke amesema wimbi la watoto kukimbilia mitaani limekuwa kubwa na sababu zikiwa ni pamoja na kutetereka kwa wanandoa na hivyo kutoa rai kwa viongozi wa dini kuongeza juhudi za kutoa elimu na mafunzo kwa vijana kabla ya kuingia kwenye ndoa.


“Tunataka jambo hili la malezi ya ndoa lipewe kipaumbele kwenye uislamu na liwe ni agenda yetu ya kudumu. Hii itasaidia kupunguza mitafaruku kwenye ndoa, kusaidia zisivunjike na hivyo wanandoa kuona umuhimu na wajibu wa kulea watoto wao kwa misingi bora”, amesema Sheikh Kabeke.


Akifungua kongamano hilo, Katibu Tawala Mkoa Mwanza, Ngusa Samike amesema Serikali kupitia vyombo vyake inaweka jitihada za kuhakikisha inadhibiti vitendo vya ukatili wa kijinsia katika jamii na kwamba yeyote atakayebainika kutenda vitendo hivyo ikiwemo vipigo kwa wanawake hatua za kisheria zitachukuwa dhidi yake bila kujali nafasi yake.


“Nimesikia hapa kuna mama mmoja anatendewa ukatili na mmewe na hatua hazijachukuliwa kutokana na nafsi aliyonayo, naomba nipate hiyo taarifa ofisini kwangu na tutachukua hatua haraka, sisi viongozi hatuko juu ya sheria na hatupaswi kutenda ukatili kwa wenza wetu” ameonya Samike.


Wakati hayo yakijiri, tayari Serikali mkoani Mwanza kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo Kamati ya MTAKUWWA Mkoa Mwanza imeanza kutafuta mbinu bora na rafiki za kuwaondoa watoto wanaoishi mitaani pamoja na kutokomeza utoro katika Shule za Msingi na Sekondari.
Na George Binagi-GB Pazzo, BMG
Mkurugenzi Mtendaji Shirika la KIVULINI, Yassin Ally akizungumza wakati wa kongamano hilo.
Kongamano hilo ni sehemu ya kampeni ya malezi bora, tabia njema na misingi ya ndoa iliyoasisiwa na BAKWATA Mkoa Mwanza kupitia idara za Tabliigh na Daawa kwa kushirikiana na Shirika la KIVULINI ikilenga kutoa elimu ya kutokomeza ukatili wa kijinsia katika jamii.
Sheikh wa BAKWATA Mkoa Mwanza, Sheikh Hassan Kabeke akizungumza kwenye kongamano hilo.
Kongamano hilo limeambatana na jumbe mbalimbali ikiwemo “epuka unyanyasi wa jinsia, epeuka liwatwi (ulawiti), simama kuhakikisha Mwanza haina watoto wa mitaani, unyanyasi wa jinsia ni ukatili wa wazi. BAKWATA sisi tunapinga, Kivulini sisi tunapinga, wewe je?”
Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake BAKWATA Mkoa Mwanza, Amina Masenza akitoa masaha zake kwwenye kongamano hilo na kusisitiza wanandoa kuwa na maelewano hatua itakayosaidia malezi bora kwa watoto.
Mkurugenzi wa taasisi ya Nitetee, Florah Magabe akichangia mada kwenye kongamano hilo na kuhimiza jamii kutonyamazia vitendo vya ukatili wa kijinsia akisema bado kuna vitendo vya ukatili wa kijinsia katika ndoa ambapo wanawake na wanaume wote hukumbwa na vitendo hivyo na kuomba hatua kuchukuliwa kwa wanaojiuhusisha na vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Mkuu wa Kituo cha Polisi Mirongo jijini Mwanza, Charles Mawilo alitoa rai makongamano ya utoaji elimu katika jamii kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia kuwa endelevu hatua itakayosaidia elimu kufika katika jamii.


Waumini wa dini ya kiislamu jijini Mwanza wakifuatilia kongamano hilo.
Waumini wa dini ya kiislamu jijini Mwanza wakifuatilia kongamano la malezi bora, tabia njema na misingi ya ndoa lililoandaliwa na Baraza Kuu la Waislamu BAKWATA Mkoa Mwanza.
Wanahabari jijini Mwanza wakinasa matukio kwenye kongamano hilo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com