Muthoni wa Kirima almaarufu Field Marshal, akinyolewa nywele zake alizozifuga tangu mwaka 1963
**
Mpigania uhuru maarufu nchini Kenya, Muthoni wa Kirima almaarufu Field Marshal, amenyolewa nywele zake alizozifuga tangu mwaka 1963 baada ya Kenya kupata uhuru kutoka kwa wakoloni.
Tukio la mpigania uhuru huyo kunyolewa nywele zake, limetokea wikiendi iliyopita na kuzusha gumzo kubwa baada ya picha kuanza kusambaa kwenye mitandao ya kijamii zikimuonesha ‘first lady’ wa zamani na mama wa rais wa sasa, Mama Ngina Kenyatta akimnyoa nywele hizo.
Muthoni mwenye umri wa miaka 92, anafahamika zaidi kuwa mwanamgambo wa Mau Mau aliyepigana na wakoloni wa Uingereza wakati wa harakati za kudai uhuru wa Kenya.
Muthoni wa Kirima akishangilia mara baada ya kunyolewa nywele zake alizozifuga tangu mwaka 1963
Tofauti na wapiganaji wengine, baada ya kupata uhuru Muthoni hakunyoa nywele zake na kuanza kuzifuga kama moja ya alama za wapiganaji hao waliokuwa wanafuga nywele kipindi cha kupigania uhuru.
Inaelezwa kwamba katika harakati za kudai uhuru, Muthoni aliishi msituni kwa muda wa miaka saba ambapo tofauti na wenzake ambao waliwekwa kama wakuu wa upelelezi wa Mau Mau au wasambazaji wa chakula msituni, yeye alisimama mstari wa mbele vitani na kusababisha abatizwe jina la Field Marshal kutokana na ujasiri wake.
Miaka kadhaa iliyopita, Muthoni alijiapiza kwamba kamwe hatanyoa nywele hizo mpaka serikali itakaposhughulikia matakwa yake ambapo juzi wakati akinyolewa nywele hizo, alisema tayari matakwa yake yametekelezwa bila kueleza ni matakwa gani.
Social Plugin