Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MADUKA YA DAWA YASIYO SAJILIWA KUFUNGWA NCHI NZIMA


Msajili wa Baraza la Famasi Bi. Elizabeth Shekhalage

Na WAF Dar es Salaam

Wizara ya Afya kupitia Baraza la Famasi Tanzania itayafungia maduka yote ya dawa ambayo hayajasajiliwa wala kuwa na vibali na kuchukua hatua za kisheria.

Hayo yamebainishwa leo jijini Dar es Salaam na Msajili wa Baraza la Famasi Bi. Elizabeth Shekhalage wakati wa ukaguzi unaoendelea nchini kwenye maduka ambayo hayana sifa.

Bi. Shekalaghe amesema kuwa maduka yote ya dawa ambayo hayajasajiliwa na yasiyo na vibali vyenye nembo ya kielekroniki Yaani (barcode Au QR code) yakibainika yatafungwa mara moja na hatua za kisheria zitachukuliwa.

 "kwa siku ya jana tumebaini maduka ya dawa 23  ambayo hayajasajiliwa kwa mkoa wa Dar es Salaam na yote tumeyafunga, tunaendelea na zoezi la ukaguzi nchi nzima ili kuweza kubaini maduka yote ya dawa ambayo hayatambuliki na Baraza ". Bi. Shekalaghe

"Vibali vyote vya maduka ya dawa nchini sasa hivi vina nembo ya kielektroniki na tumefanya hivi ili kuweza kuwabaini watoa huduma ambao sio waaminifu".

Hata hivyo Bi. Shekalaghe amewaomba wananchi kutoa taarifa pale ambapo watakuwa na wasiwasi ama kutokuridhika  na huduma za dawa wanazozipata kwenye maduka ya dawa ili kuweza kuchukua hatua stahiki

"Tuna namba yetu ambayo unaweza kupiga bila malipo ambayo ni 08 0011 0015, tupigieni ili tuweze kuchukua hatua stahiki kwani kila mwananchi ana haki ya msingi ya kupata huduma ya dawa iliyo sahihi "Amesema 

Aidha, amewataka wananchi kuhakikisha  wanapoenda kwenye duka la dawa lazima wakute nembo ya duka la dawa muhimu na kuona cheti cha mtoa huduma chenye nembo ya kielektroniki.

Vilevile Bi. Shekalaghe amewaonya watoa huduma kuacha mara moja kutoa huduma za kitabibu katika maduka ya dawa ikiwemo kuchoma sindano na kufanya vipimo. “Si ruhusa kuchoma sindano wala kufanya vipimo vya aina yoyote  katika duka la  dawa, endapo tukikukamata hatua za kisheria zitachukuliwa "Amesisitiza.

Kwa upande mwingine Bi. Shekalaghe amewasihi watoa huduma na wamiliki wa maduka ya dawa nchini kuwa waaminifu katika utoaji wa huduma za dawa.

"Wamiliki na watoa huduma wengi wa maduka ya dawa  sio waaminifu, Hivi karibuni Tumefanya tafiti katika kaguzi zetu tumebaini kuna watoa huduma za dawa ambao wanajifanya wamesoma lakini hawajasoma"


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com