NA GODFREY NNKO
MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), Bi.Bahati Geuzye ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwezesha Mfuko wa Elimu wa Taifa unaoratibiwa na mamlaka hiyo ili kugharamia uboreshaji na ujenzi wa miundombinu ya elimu nchini.
Ameyasema hayo leo Aprili Mosi, 2022 katika Ukumbi wa Mikutano wa TEA jijini Dar es Salaam wakati akifungua semina ya waandishi wa habari iliyoangazia majukumu mbalimbali ya mamlaka hiyo.
"Tunaishukuru sana Serikali ya Awamu ya Sita, kwani kupitia Mfuko wa Elimu wa Taifa unaoratibiwa na Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), katika mwaka wa fedha 2021/2022 zaidi ya shilingi Bilioni 8.6 ziliidhinishwa kwa ajili ya kugharimia ufadhili wa miradi 160 ya kuboresha miundombinu ya elimu katika shule 151 nchini.
"Miradi hiyo inahusisha ujenzi wa madarasa 210 katika shule 70, maabara mbili za sayansi katika shule za sekondari zenye mahitaji maalum, matundu ya vyoo 2,040 katika shule 80, vifaa vya kujifunzia na kufundishia na uendelezaji wa miundombinu katika shule za watoto wenye mahitaji maalum,"amesema.
Kuhusu Mfuko wa Elimu
Sheria Na. 8 ya Mfuko wa Elimu ya Mwaka 2001 pamoja na marekebisho yake (2013), imeainisha madhumuni na majukumu makuu ya Mamlaka ya Elimu Tanzania ikiwemo kufadhili miradi ya elimu katika ngazi zote.
Mratibu Msaidizi Mradi wa Kuendeleza Ujuzi (TEA), Bw.Lusungu Kaduma akichangia jambo katika Semina ya waandishi wa habari kuhusu majukumu ya TEA iliyofanyika katika Ofisi za Makao Makuu ya TEA leo Aprili Mosi, 2022 jijini Dar es Salaam.
Lengo likiwa ni kuinua kiwango cha ubora wa elimu na kuongeza upatikanaji wake kwa usawa kulingana na mipango na sera za kitaifa kwa lengo la kukidhi mahitaji ya kijamii na kiuchumi.
Wakati huo huo, Bi.Geuzye amebainisha kuwa, tangu kuanzishwa kwa mamlaka hiyo, imefadhili miradi 3,314 ya elimu yenye thamani ya shilingi bilioni 212.64 ambapo shilingi Bilioni 200.38 ni ruzuku na shilingi Bilioni 12.26 ni mikopo nafuu kwa shule za awali, msingi, sekondari, vyuo vya ualimu, vyuo vya ufundi na vyuo vikuu.
"Pia inajumuisha ujenzi wa mabweni 73, vyumba vya madarasa 1,050, matundu ya vyoo 5,880 na nyumba za walimu 560 katika shule 791 za msingi na sekondari, ukarabati wa shule 17 za sekondari kongwe,"amesema.
Katika hatua nyingine, Bi.Geuzye amesema, TEA ambayo ni mamlaka ya Serikali iliyopo chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia mbali na miradi ya Mfuko wa Elimu wa Taifa,mamlaka hiyo inatekeleza mradi wa miaka mitano (2016/17-2020/21) unaotoa ruzuku za utekelezaji wa miradi ya kuendeleza ujuzi kutoka kwenye Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi (Skills Development Fund-SDF).
Afisa Habari wa TEA, Bi.Eliafile Solla akiwasilisha mada kwenye semina ya waandishi wa habari kuhusu majukumu ya TEA iliyofanyika katika Ofisi za Makao Makuu ya TEA leo Aprili Mosi, 2022 jijini Dar es Salaam.
Mwaka 2017, TEA ilipewa jukumu la kusimamia na kuratibu Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi (SDF) ikiwa ni sehemu ya Programu ya Kuendeleza Elimu ya Ujuzi na Mafunzo ya Stadi za Kazi zenye Kuleta tija katika Ajira (Education and Skills for Productive Jobs-ESPJ) na Mpango Mkakati wa Kitaifa wa Kukuza na Kuendeleza Ujuzi nchini (National Skills Development Strategy-NSDS).
“Mfuko wa SDF unalenga kuendeleza ujuzi kwa Watanzania ili kuwawezesha kujiajiri au kuajiriwa kwa urahisi na kuchangia uchumi wa Taifa. Mpango umelenga kunufaisha vijana 38,000,”amesema Mkurugenzi Mkuu huyo.
Kaimu Mkurugenzi Huduma za Taasisi (TEA), Bi. Tija Ukondwa akifuatilia semina ya waandishi wa habari kuhusu majukumu ya TEA iliyofanyika katika Ofisi za Makao Makuu ya TEA leo Aprili Mosi, 2022 jijini Dar es Salaam.
Bi.Geuzye amefafanua kuwa, kupitia mfuko huo ujuzi kiasi cha sh.milioni 385.8 zinatarajiwa kunufaisha vijana 1,018 katika mpango wa Uanagenzi na Utarajari (Internship and Apprenticeship) katika sekta za Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, Utalii na huduma za Ukarimu, Nishati, Ujenzi na Uchukuzi.
Aidha, amaesema Mfuko wa SDF pia unafadhili mafunzo kwa wanufaika 4,000 kutoka kaya maskini na makundi maalum (Bursary Scheme) hadi Agosti 2021, jumla ya wanufaika 1,627 walipata mafunzo katika Awamu ya Kwanza ya Mpango huo huku Awamu ya Pili ya Mpango wa Ufadhili inatarajiwa kuanza mwezi huu wa Aprili 2022, ambapo wanufaika 2,373 wanatarajiwa kupata mafunzo kabla ya Juni, 2022.
Kaimu Mkurugenzi wa Miradi na Utafutati Rasilimali (TEA), Bi. Anna Makundi akifuatilia semina ya waandishi wa habari kuhusu majukumu ya TEA iliyofanyika katika Ofisi za Makao Makuu ya TEA leo Aprili Mosi, 2022 jijini Dar es Salaam.
Pia ameeleza kuwa Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi pia uko katika hatua za mwisho kuanza kutekeleza ufadhili wa mafunzo ya kiubunifu kwa njia ya mtandao (innovative training through e-learning) ambapo umelenga wanufaika 4,305 ifikapo Juni 2022.
Amesema, zaidi ya shilingi Bilioni 2.3 zitatumika kufadhili mradi huo ambapo zinatokana na ruzuku.
Afisa Utafutaji Rasilimali na Hamasa Mkuu (TEA), Bw.Hamza Hassan akichangia jambo katika semina ya waandishi wa habari kuhusu majukumu ya TEA iliyofanyika katika Ofisi za Makao Makuu ya TEA leo Aprili Mosi, 2022 jijini Dar es Salaam.
TEA nini?
Mamlaka ya Elimu Tanzania (Tanzania Education Authority-TEA) ilianzishwa kwa Sheria ya Bunge ya Mfuko wa Elimu Na. 8 ya mwaka 2001 chini ya kifungu 5 (1) pamoja na marekebisho yake (2013) kwa lengo la kuratibu uendeshaji wa Mfuko wa Elimu.Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu Tanzania, Bi.Bahati Geuzye akiwa pamoja na watuumishi wa TEA wakipata picha ya pamoja na waandishi wa habari katika semina ya waandishi wa habari kuhusu majukumu ya TEA iliyofanyika katika Ofisi za Makao Makuu ya TEA leo Aprili Mosi, 2022 jijini Dar es Salaam.
Madhumuni ya Mfuko wa Elimu ni kuongeza nguvu za Serikali katika kugharamia miradi ya elimu ili kuinua ubora wa elimu na upatikanaji wake kwa usawa, katika ngazi zote za Elimu kwa Tanzania Bara na Elimu ya Juu kwa Tanzania Zanzibar.