WATOTO 349,007 KUPATIWA CHANJO YA POLIO SHINYANGA...RC MJEMA ATAKA WAPOTOSHAJI WAPUUZWE


 Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Sophia Mjema akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano Aprili 27,2022

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Sophia Mjema, akizungumza na waandishi wa habari mkoani humo.

Mwakilishi kutoka Wizara ya Afya mkoani Shinyanga Aziz Sheshe, akielezea umuhimu wa chanjo ya Polio.

Mratibu wa chanjo mkoani Shinyanga Timoth Sosoma, akielezea namna walivyojipanga kutoa chanjo ya Polio mkoani humo na kufikia lengo.

Kikao kikiendelea.

****

Na Marco Maduhu, SHINYANGA

SERIKALI mkoani Shinyanga, inatarajia kutoa chanjo ya Polio kwa watoto 349,007 , ili kuimarisha kinga za miili yao, na kuwakinga dhidi ya ugonjwa wa Polio wa kupooza.
 
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Sophia Mjema, amebainisha hayo leo Aprili 27, 2022 wakati akizungumza na vyombo vya habari.

Amesema, chanjo hiyo itatolewa kwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano, ambao ndiyo wameonekana kuathiriwa zaidi na ugonjwa huo wa Polio.

"Kampeni hii ya utoaji chanjo ya Polio itatolewa nyumba kwa nyumba, maeneo ya masoko, stendi za mabasi na mashuleni," amesema Mjema.

"Chanjo hii ya Polio ni salama haina madhara yoyote, nawaomba wazazi watoe ushirikiano wa kutosha, ili watoto wao wapate chanjo na kuendelea kuwa salama dhidi ya ugonjwa huu ambao ni hatari," ameongeza Mjema.

Aidha, amesema chanjo hiyo ya Polio siyo ngeni hapa nchini Tanzania, hivyo wananchi wasiwe na wasiwasi na kupuuza upotoshaji wowote, ili kuendelea kuwalinda watoto wao dhidi ya ugonjwa huo.

“Natoa wito kwa wananchi wa mkoa wa Shinyanga kupuuza upotoshaji wa aina yoyote ile kwenye kampeni hii ya utoaji wa chanjo ya Polio, bali watoe ushirikiano kwa wataalamu ambao watafika kwenye maeneo yao kwa ajili ya kutoa chanjo ya Polio,”amesema Mjema.

“Chanjo ya Polio ndio kinga pekee inayoweza kumlinda mtoto dhidi ya ugonjwa huu hatari, na chanjo ni salama haina madhara yoyote na mtoto anaweza kupata chanjo ya polio hata mara nne au zaidi ili kuongeza kinga zaidi na kumlinda na ugonjwa huu wa polio wa kupooza,”anafafanua zaidi.

Naye Mwakilishi kutoka Wizara ya Afya mkoani Shinyanga Aziz Sheshe, amewasihi watanzania wasipuuze kuwapatia watoto wao chanjo hiyo ya Polio, kwa sababu ni muhimu katika kuwalinda na ugonjwa huo hatari.

Amesema mlipuko wa ugonjwa wa Polio (kupooza) ulianzia nchini Malawi Februari 17 mwaka huu, na nchi hiyo inapakana na mikoa ya Tanzania, ambayo ni Mbeya, Ruvuma, Njombe, na Songea, hali ambayo ni hatari ugonjwa huo kusambaa hapa nchini.

Kwa upande wake Mratibu wa Chanjo mkoani Shinyanga Timoth Sosoma, amesema wameshajipanga vyema na timu yake, kwa kutoa Chanjo hiyo ya Polio na kufikia malengo ya mkoa huo kwa kuchanja watoto hao 349,007.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post