Kamishina wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima (TIRA), Dk. Baghayo Saqware, akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa Miongozo ya Bima 2022 yenye kufuata misingi ya dini ya kiislam (TAKAFUL).
**
WATEJA wa Benki ya CRDB sasa wanaweza kupata huduma za Bima zinazofata misingi ya Shariah, ijulikanayo kama Takaful baada ya kuzinduliwa kwa miongozo mipya ya Bima 2022.
Kuazishwa kwa huduma za bima za Takaful kunaongeza muhimili wa pili katika mfumo wa fedha unaofata misingi ya kiislam katika soko, hii imekuja baada ya takriban miaka 14 tokea huduma za kibenki zinazofata misingi ya kiislam kuanzishwa nchini, hii inaashiria muendelezo wa ukuaji wa mfumo wa fedha wa kiislam Tanzania.
Kwa upande wa huduma za kibenki zinazofata misingi ya Shariah, kwa mara ya kwanza huduma hizi zinapatika nchi nzima kupitia CRDB Al Barakah Banking, ambazo zilianzishwa mwishoni mwa mwaka jana.
Benki hiyo imezitaka Kampuni za Takaful kuwekeza fedha katika misingi inayofata Shariah, hivyo basi benki hiyo imeyahakikishia makampuni ya Takaful kwamba, CRDB Al - Barakah ipo tayari na imejidhatiti kuwapatia fursa za uwekezaji unaofuata misingi ya Shariah.
Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi huo, Mkuu wa Kitengo cha CRDB Al-Barakah Banking, Rashid Rashid, alisema.
“Sisi kama Benki ya CRDB, na hususan kupitia huduma zetu za Al Barakah pamoja na kitengo cha BIMA cha CRDB, tuko tayari kufanya kazi na taasisi zitakazojisajili kutoa huduma za TAKAFUL kwa namna mbalimbali.”
Kwa sasa “tumefarijika sana kwamba sasa mwanga umefunguka wa kuwawezesha wateja wetu kupata huduma za BIMA zinazofata misingi ya Shariah, yaani Takaful.” Alisema Rashid.
Katika mfumo wa fedha unaofata misingi ya Halal au Shariah, kuna mihimili mikuu mitatu ambayo ni Islamic Banking, Islamic Insurance pamoja na Islamic money markets & capital markets (Masoko ya fedha na mitaji).
Ili mfumo wa kifedha unaofata Shariah ukamilike bado kulikuwa kunatakiwa uwepo wa Islamic Insurance (Takaful) pamoja na masoko ya fedha na mitaji, ambapo mihimili hii miwili ya mwisho haikuwepo na hivyo kupelekea benki zinazotoa huduma zinazofata Shariah kufanya miamala yake ya BIMA kwa dharura ya kutumia BIMA za conventional.
Ujio wa Takaful sio tu unaongeza wigo wa huduma za bima nchini, bali utazisaidia benki zinazofuata misingi ya Shariah kukidhi vigezo vya kishariah katika utoaji wa huduma zake.
"Wateja wote wa CRDB Al Barakah watatumia huduma za TAKAFUL katika mahitaji ya BIMA, kwa sababu hapo awali tulikua tunatumia bima za conventional kwa mlango wa dharura. Kwa ujio wa Takaful, mlango wa dharura umefungwa, kwa hiyo tutatumia Takaful." alisema Rashid.
Mkuu wa Kitengo cha CRDB Al-Barakah Banking, Rashid Rashid, akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa Miongozo ya BIMA 2022 yenye kufuata misingi ya dini ya kiislam (TAKAFUL) uliofanyika jijini Dar es Salaam na kudhaminiwa na Benki ya CRDB. (Na Mpigapicha Wetu).
Mkuu wa Kitengo cha CRDB kinachosimamia masuala ya BIMA, Moureen Majaliwa, akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Miongozo Mipya ya BIMA ya TAKAFUL.
Kamishina wa Mamlaka ya Usimamizi wa BIMA (TIRA), Dk. Baghayo Saqware, akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi rasmi wa Miongozo ya BIMA 2022 yenye kufuata misingi ya dini ya kiislam (TAKAFUL).
Social Plugin