Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia mwanamke aitwaye Riziki Henry (22) Mkazi wa Nditu Wilaya ya Rungwe kwa tuhuma za mauaji ya mume wake aitwaye Ayubu Aron (33) Mkazi wa Nditu.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Ulrich Matei tukio hilo limetokea tarehe 02.04.2022 majira ya saa 05:00 alfajiri huko Nditu, Kata ya Suma, Tarafa ya Ukukwe, Wilaya ya Rungwe, Mkoa wa Mbeya AYUBU ARON [33] Mkazi wa Nditu alijeruhiwa kwa kupigwa na kitu butu kichwani na kuchomwa kitu chenye kali kisogoni na mke wake aitwaye Riziki Henry (22)Mkazi wa Nditu.
"Baada ya tukio hilo, mhanga alikimbizwa Hospitali ya Wilaya ya Rungwe – Makandana kwa matibabu lakini mnamo tarehe 02.04.2022 majira ya saa 17:30 jioni alifariki dunia akiwa anaendelea kupatiwa matibabu Hospitalini hapo",amesema Kamanda huyo wa Polisi.
Amesema Chanzo cha tukio ni ugomvi uliotokana na mwanamke ambaye ni mtuhumiwa kuchelewa kurudi nyumbani na alipoulizwa ndipo ulizuka ugomvi uliopelekea kifo cha mwanaume.
Mwili wa marehemu umehifadhiwa Hospitali ya Wilaya ya Rungwe – Makandana kwa uchunguzi wa kitabibu. Upelelezi wa shauri hili unaendelea na mara baada ya kukamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani.
Social Plugin