Mfano wa mkanda wa suruali
Na Walter Mguluchuma - Katavi
Mwendesha pikipiki maarufu bodaboda aitwaye Idrisa Salum Milundiko (24) Mkazi wa Mtaa wa Nsemlwa Manispaa ya Mpanda Mkoa wa Katavi amekutwa amefariki dunia kwa kujinyonga kwa kutumia mkanda wake wa saruali na kuacha ujumbe kwa ndugu zake kuwa ana matatizo mengi ya kimaisha.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi Ally Makame Hamad amewaambia waandishi wa habari kuwa mtu huyo amejinyonga juzi majira ya saa saba na nusu mchana kwenye kijiji cha Kasokola.
Amesema chanzo cha mtu huyo kujinyonga inaonyesha ni kutokana na msongo mkubwa wa mawazo aliyokuwa nayo kutokana na hali ya maisha yake kuona kuwa hayaendi vizuri.
Amebainisha kuwa marehemu alitoweka nyumbani kwao tangu tarehe nane ya mwezi huu wa nne huku akiwa ameacha ujumbe mfupi wa maandishi kwa ajili ya kuwaachia familia yake ya kuhusiana na tukio ambalo anataka kulifanya la kujinyonga .
Kamanda Hamad amesema kuwa ujumbe huo wa maandishi uliokuwa umeandikwa kuwa "Kaka mimi naenda kujinyonga kwani nina matatizo mengi yanayonisonga ya maisha ambayo yamenishinda kuyatatua".
Hivyo kaka mimi nakwenda kujinyonga na mwili wangu popote pale mtakapoupata baada ya kuwa nimejinyonga upelekwe kwa mjomba wangu ambaye anaishi kwenye Mtaa wa Makanyagio Manispaa ya Mpanda".
Amesema baada ya kuwa ameacha ujumbe huo hakuonekana tena hadi hapo Aprili 13,2022 alipokutwa akiwa amejinyonga porini kwenye mapori ya kijiji cha Kasokola Manispaa ya Mpanda kwa kutumia mkanda wake wa suruali.
Mwili wa marehemu umefanyiwa uchunguzi wa kidaktari na wamekabidhiwa ndugu kwa ajili ya kuendelea na taratibu za majeshi yanayotarajiwa kufanyika wakati wowote kwenye makaburi ya Mwangaza.