Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

GGML YATOA SH MILIONI 50 KWA HOSPITALI YA CCBRT

Meneja Uhusiano na Mawasiliano wa Kampuni ya GGML, Stephen Mhando (kulia) akikabidhi hundi ya Sh milioni 50 iliyotolewa na kampuni hiyo kuunga mkono juhudi za hospitali ya CCBRT katika utoaji huduma za afya ya uzazi. Kushoto na Mkurugenzi wa Huduma za kitabibu katika Hospitali hiyo ya CCBRT, Dk. Cyprian Ntomoka na katikati ni Mkuu wa Idara ya Masoko na Wateja kutoka CCBRT, Sophia Shuma.

***

Na Mwandishi Wetu - Dar es salaam

KAMPUNI ya AngloGold Ashati kupitia Mgodi wake wa dhahabu Geita (GGML) imetoa kiasi cha Sh milioni 50 kwa Hospitali ya CCBRT ili kusaidia na kuboresha huduma za afya ya uzazi.


Akizungumza juzi jijini Dar es Salaam katika hafla ya kukabidhi hundi kwa niaba ya AngloGold Ashanti, Meneja Uhusiano na Mawasiliano wa Kampuni ya GGML, Stephen Mhando alisema msada huo ni moja ya majukumu ya kampuni hiyo kutekeleza mpango wake wa Uwajibikaji kwa Jamii.

Alisema GGML inaunga mkono mipango ya serikali na wadau wengine kuhakikisha kwamba watu wote wanaishi kwa amani na ustawi, jambo ambalo linawezekana ikiwa watu wengi wana afya njema.

Alisema mchango huu wa Sh milioni 50 unakamilisha mojawapo ya maadili ya msingi ya kampuni yetu katika kuhakikisha kuwa kunakuwa na mustakabali endelevu kwa jamii.

“GGML inatekeleza kikamilifu miradi mbalimbali ya kijamii ambayo imesaidia pia kuboresha za afya. Kwa kuanzia, malengo yetu yalijikita katika kupunguza maradhi ya malaria nchini ambapo GGML imeungana na wadau mbalimbali kuhudumia meli tiba inayofahamika kwa jina la Jubilee Medical Boat, ambayo inasafiri kati ya visiwa vya Ziwa Victoria ikitoa huduma mbalimbali za afya.

“Pia GGML kwa kupitia fedha za mfuko wa Uwajibika wa kampuni kwa jamii (CSR), mwaka jana ilisaidia ujenzi wa zahanati saba katika Halmashauri ya Mji wa Geita, kukamilika kwa idara 14 za wagonjwa wa nje na vituo vya afya vitatu, utoaji wa vifaa tiba pamoja na magari matatu ya kubebea wagonjwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita.

“Zaidi ya hayo Kampuni yetu pia imesaidia kukamilika kwa idara tano za wagonjwa wa nje katika Wilaya ya Mbogwe na moja ya ziada Bukombe,” alisema.


Aliongeza kuwa takribani muongo mmoja, kampuni ya GGML kwa kushirikiana na kampuni ya Rafiki Surgical Mission kutoka Australia ilisaidia kutoa upasuaji bure kwa takriban watu wazima na watoto 2,000 kutoka vijiji mbalimbali mkoani Geita ambao walizaliwa na tatizo la mdomo sungura.


“Oktoba mwaka jana, GGML ilitia saini mkataba wa makubaliano wenye thamani ya Dola za Marekani 120,000 ili kuongeza msaada kwa boti au meli ya matibabu kwenye Ziwa Victoria ambapo ufadhili wa GGML utadumu tena kwa miaka mitano ijayo hadi 2026,” alisema.

Aidha, aliishukuru CCBRT kwa kuwa mshirika wa kweli wakati kampuni hiyo ikiendelea kutoa huduma maeneo mbalimbali nchini.

“Kampuni ya AngloGold Ashanti kupitia GGML tunashirikiana kila mara na mashirika yenye malengo kama yetu ili kuboresha na kuhakikisha huduma bora za kijamii zinawafikia watanzania wote.

“GGML itaendelea kushirikiana na serikali, jamii na wadau wengine kote nchini kuunga mkono utekelezaji wa malengo ya Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2025, pamoja na mipango mikakati mingine ya muda mrefu ya maendeleo na kuongeza uwekezaji kwa nchi,” alisema.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Huduma za kitabibu katika Hospitali hiyo ya CCBRT, Dk. Cyprian Ntomoka alisema msaada huo utaendelea kuboresha utoaji wa huduma za hospitali hiyo ambazo hugusa maisha ya watu duni wenye ulamavu wa aina mbalimbali.

“Tunatoa huduma kwa akina mama wajawazito wenye matatizo mbalimbali kama vile ulemavu. Tunatoa huduma kwa wanawake wenye matatizo ya fistula.

“Kwa hiyo GGML imetuongezea wigo mpana wa kutekeleza malengo ya CCBRT kutoa huduma kwa watu wengi zaidi.

“Pia kuna wale wenye matatizo sugu ya fistula ambayo yamewasababishia kupoteza watoto wawili au watatu. Hao pia tunawahudumia. CCBRT tupo kwa ajili ya kuwapatia huduma wale watu maskini ambao hawana uwezo wa kupata huduma za kiafya,” alisema.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com