Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

GGML YALIPA BILIONI 4 KWA HALMASHAURI MBILI GEITA

Makamu wa Rais wa AngloGold Ashanti – GGML anayeshughulikia nchi za Tanzania na Ghana, Simon Shayo

Na Mwandishi wetu

KATIKA kuunga mkono na kutimiza wajibu wake wa kulipa kodi na tozo mbalimbali kwa Serikali, Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) imelipa zaidi ya Shilingi bilioni nne kwa Halmashauri mbili za Geita Mji na Geita Wilaya kwa kipindi cha mwezi Julai 2021 mpaka mwezi Machi 2022.


Malipo hayo ni tozo ya huduma ambayo inalipwa kwa halmashauri husika.

Akizungumzia malipo hayo kwa halmashauri husika Mjini Geita hivi karibuni, Makamu wa Rais wa AngloGold Ashanti – GGML anayeshughulikia nchi za Tanzania na Ghana, Simon Shayo alisema kampuni hiyo inatambua na kuthamini umuhimu wakulipa kodi na tozo mbalimbali kwa Serikali.


Alitaja tozo hizo kuwa ni pamoja na ya huduma kwa kuwa mapato hayo yanaiwezesha serikali katika kuwaletea maendeleo wananchi.


“Mchango huu unaonesha dhahiri jinsi kampuni yetu ilivyo mstari wa mbele katika kulipa kodi na tozo mbalimbali kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wa Geita ikiwa pia ni mwitikio wetu wa kutii na kutekeleza sheria za nchi ya Tanzania,” alisema Shayo.


“Mbali na kodi na tozo mbalimbali zinazolipwa moja kwa moja kwa Serikali kuu na halmashauri zetu, Kampuni ya GGML inao mpango mahususi wa kuchangia maendeleo ya jamii kupitia utaratibu wa kurudisha kwa jamii, yaani Corporate Social Responsibility (CSR).


“Kampuni imejikita katika kusaidia jamii kwa kuboresha miundombinu na huduma hususan katika nyanja za afya, elimu, maji na barabara.

“Kampuni pia inao mpango wa kusaidia kukuza fursa za kiuchumi kwa wafanyabiashara wazawa ambapo kampuni hiyo imetumia jumla ya Sh bilioni 863 katika manunuzi ya bidhaa na huduma kutoka kwa kampuni za kitanzania ambapo jumla ya sh bilioni 69 zimetumika mjini Geita kwa kipindi chai mwaka 2021,” alisema.


Aidha, alisema katika kuendeleza biashara za Kitanzania kwenye mnyororo wa thamani ndani ya mgodi, GGML imeshirikiana na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) na kuwajengea uwezo wafanyabiashara zaidi ya 500 kutoka Geita kwa kuwapatia mafunzo na ujuzi mbalimbali ili waweze kushindana vyema na wafanyabiashara wengine wa Kitanzania katika mchakato wa manunuzi.


“Lakini pia tunafarikija kwa kuwa Serikali na wadau wetu wengine wanatambua mchango huu ambapo mapema mwaka huu, GGML iliibuka mshindi wa jumla katika kampuni zinazofanya vizuri kwenye sekta ya madini nchini Tanzania kwa mwaka wa fedha 2020/2021.

“GGML ilinyakua tuzo katika vipengele vya uwajibikaji wa kampuni kwa jamii, mazingira, usalama, mlipaji bora wa mapato (kodi) na uendelezaji wazawa, ikiwa ni mara ya pili mfululizo” alisema Shayo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com