Kwenye picha ni wataalam wa kampuni ya Meta wakiwa na viongozi wa TRA.
**
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imekutana na wataalam wa kampuni ya Meta inayomiliki mtandao wa instagram, whatsapp na facebook kujadili namna ya kukusanya kodi kupitia huduma zao nchini.
TRA imefanya mazungumzo ya awali na kampuni ya Meta kuhusu namna ya kutoza kodi katika huduma zao nchini. Mazungumzo hayo yamefanyika jijini Dar es Salaam.
TRA wametoa taarifa hiyo kupitia ukurasa wao wa twitter.
Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA,Richard Kayombo amesema kuwa zoezi hilo litakapokamilika, kodi hiyo haitatozwa kwa wale wanaotumia mitandao kwa matumizi yasiyoingiza kipato.
“ Watanzania wawe watulivu, hatutawatoza watu ambao hawafanyi biashara mitandaoni. Sisi tutakaowatoza hapo mbeleni ni wale wanaofanya biashara kwenye mitandao na ndio maana timu ya wataalamu wa Kampuni ya Meta wamefanya mazungumzo ya awali na TRA kuhusu namna ya kutoza kodi katika huduma zao nchini,” ameeleza Kayombo.
"Baada ya mazungumzo hayo ambayo Meta wametupa uzoefu wao katika kuchangia kodi kwenye nchi kama Kenya, Nigeria na Afrika Kusini, sasa Serikali inaendelea kuangalia upande wa sheria zetu ili tuone namna gani tunaweza kuanza kukusanya kodi kwa wale wanaofanya biashara mitandaoni",ameongeza
Mpaka Desemba 2021,Tanzania ina watumiaji zaidi ya milioni 29 wanaotumia intaneti.