Mkuu wa mkoa wa Arusha, John Mongela, akiwahutubia wakazi wa Arusha, kwenye kilele cha siku ya upandaji miti mkoa wa Arusha, maadhimisho yaliyofanyika kwenye shule ya msingi Enaboishu Academy, halmashauri ya Arusha, wilaya ya Arumeru.
Na Rose Jackson,Arusha
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. John Mongella amewaagiza wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri zote za mkoa wa Arusha, kuweka mkakati kwa kushirikiana na wadau kuandaa miche milioni 1.5, kwa kila halmashauri kwa ajili ya kuipanda kwa mwaka, ili kufikia lengo la mkoa la kupanda miti milioni 10.5 kwa mwaka.
Mongela maetoa maelekezo hayo, kwenye maadhimisho ya kilele cha upandaji miti mkoa wa Arusha, yaliyofanyika kwenye viwanja vya shule ya msingi Enaboishu Academy, halmasahuri ya Arusha na kuwataka wakuu wa wilaya na wakurugenzi kuandaa mkakati wa kuoanda miti milioni 1.5 kwa kila halmashauri kwa mwaka.
"Mkakati wetu ni huu, kila halmashauri kupanda miti milioni moja 1.5 kwa mwaka, tunataka kila mdau, wadau wa mistu, watupe miche ya miti ili kufikia lengo la mkoa la kupanda miti milioni 10.5 ifikapo mwezi Aprili 2023", amesisitiza Mongela.
Aidha amezitaka taasisi zote za serikali, taasisi binafsi na zile za dini kuwawezesha watu wanaowahudumia, kuhakikisha kila watu wawili wanapanda mti mmoja sambamaba na kuuhudumia mti huo, kwa kipindi cha mwaka mzima na kuongeza kuwa, kila shule iwape jukumu kila wanafunzi wawili wapande mti mmoja, kila kanisa na msikiti waumini wawili wapande mti mmoja na kuutunza mpaka ukue.
"Tunafahamu miti ndio chanzo kikubwa cha maji, miti ni chanzo cha hewa safi, tumeshuhudia mabadiliko ya hali ya hewa, kwa sababbu ya uharibifu wa mazingira, tusifanye uzembe, watalamu na wadau tusidieni kubadilisha maeneo makame kwa kupanda miti ya kutosha, ili kuyafanya mazingira yetu yatutunze", ameweka wazi mkuu huyo wa mkoa.
Naye Mkurugenzi mtendaji, halmashauri ya Arusha, Seleman Msumi, ameahidi kutekeleza agizo hilo la mkuu wa mkoa, kwa kushirikiana na wadau, kwa kuhakikisha wanafikia lengo la kupanda miti milioni 1.5, huku akiwataka wadau kuelekeza nguvu kuwekeza kwenye upandaji miti kwenye taasisi zote za Umma hususani kwenye shule zote za serikali na binafsi.
Kauli mbiu ni "Mti wangu, Taifa langu, Mazingira yangu, Kazi Iendelee".