Mkurugenzi wa wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Dkt. Yusuf A.Ngenya akizungumza katika mkutano wa 24 wa Kamati ya Wakuu wa Mashirika ya Viwango Afrika Mashariki( EASC) uliofanyika kwa siku tatu kati ya Aprili 27 hadi 29,2022,Jijini Arusha
Meneja Viwango ( TBS) Mhandisi Yona Afrika Mwampagatwa aliyechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya kusimamia Uandaaji Viwango Afrika Mashariki ( EAC/SMC)
*********************
NA MWANDISHI WETU, ARUSHA
Shirika la Viwango Tanzania (TBS), limeshiriki mkutano wa 24 wa Kamati ya Wakuu wa Mashirika ya Viwango Afrika Mashariki( EASC) ili kujadili masuala ya viwango kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Akizungumza katika Mkutano huo wa siku tatu kati ya Aprili 27 hadi 29,2022,Jijini Arusha, Mkurugenzi wa TBS, Dkt. Ngenya A.Y amesema mkutano huo uliojumuisha wakurugenzi wa viwango kutoka nchi za EAC ni muhimu kwa ajili ya kuonisha viwango vya ubora wa bidhaa ili kuwezesha biashara kati ya nchi hizo.
"Nchi hizi zimeshafanyia kazi changamoto mbalimbali za viwango vya ubora wa bidhaa katika mipaka na hivi karibuni nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) imeingia ndani ya EAC hivyo ni jukumu letu kuhakikisha biashara zinakuwa ikiwemo uboreshaji wa viwango vya ubora kwa pamoja". Amesema Dkt.Ngenya.
Aidha Dkt.Ngenya amesema kujiunga kwa DRC ndani ya EAC ni fursa kubwa za kibiashara hivyo ni vema kuweka ubora wa viwango dhabiti ili kila nchi iweze kunufaika.
Amesema kupitia mkutano huo watahakikisha hakuna vikwazo vya kibiashara vinavyoweza kutokea baina ya nchi hizo ikiwemo pia DRC iliyopata fursa ya kujiunga EAC.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la Ukadiriaji wa Ubora wa Bidhaa nchini Kenya (KEBS) Bw.Bernard Njiriani amesema mashirika ya viwango yanajadiliana kuhusu uoanishaji wa viwango ili kuongeza biashara na kila nchi iweze kunufaika pamoja na kuvutia wawekezaji.
Amesema changamoto zote za viwango ndani ya EAC zinaendelea kutatuliwa ili kuhakikisha uchumi unakua na wawekezaji wanawekeza katika nchi wanachama kutokana na ubora wa viwango vya bidhaa kwa kila nchi.
Hata hivyo kupitia mkutano huo Kamati ilimchagua Mhandisi Yona Afrika Mwampagatwa kutoka TBS kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kusimamima Uandaaji wa Viwango ya Afrika Mashariki ( SMC) na Bw. Jerome Ndahimana kutokea Shirika la Viwango Rwanda kuwa Katibu kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia April 2023.
Vilevile Kamati ilimpendekeza Mhandisi Yona Afrika Mwampagatwa kutoka TBS kuwania nafasi ya uwenyekiti katika ngazi ya Bara la Afrika.
Tanzania iliwasilishwa vema na TBS sambamba, Taasisi ya Viwango Zanzibar (ZBS)na Wakala wa Vipimo (WMA) na imeahidi kuasili viwango vilivyoanishwa ndani ya muda ili kuwezesha biashara.
Social Plugin