Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Mhandisi Kundo Mathew (Mb) akizungumza wakati akifungua kikao kazi cha Wakaguzi wa Ndani wa Mkoa kwa lengo la kuandaa mpango kazi wa ukaguzi wa operesheni ya Anwani za Makazi kilichofanyika leo tarehe 08 Aprili 2022 jijini Dodoma.
Mkurugenzi wa Idara ya TEHAMA wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mulembwa Munaku akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo wakati wa kikao kazi cha Wakaguzi wa Ndani wa Mikoa yote 31 nchini cha kuandaa mpango kazi wa ukaguzi wa operesheni ya Anwani za Makazi kilichofanyika leo tarehe 08 Aprili 2022 jijini Dodoma.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Anthony Mtaka akizungumza wakati wa kikao kazi cha Wakaguzi wa Ndani wa Mikoa yote 31 nchini kwa lengo la kuandaa mpango kazi wa ukaguzi wa operesheni ya Anwani za Makazi kilichoandaliwa na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na kufanyika kwa siku mbili tarehe 08 hadi 9 Aprili 2022 jijini Dodoma.
Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, CPA, Joyce Christopher akizungumza wakati wa kikao kazi cha Wakaguzi wa Ndani wa Mikoa yote 31 nchini cha kuandaa mpango kazi wa ukaguzi wa operesheni ya Anwani za Makazi kilichofanyika leo tarehe 08 Aprili 2022 jijini Dodoma.
Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Mhandisi Kundo Mathew (kulia) akiteta jambo na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Anthony Mtaka wakati wa kikao kazi cha Wakaguzi wa Ndani wa Mikoa yote 31 nchini cha kuandaa mpango kazi wa ukaguzi wa operesheni ya Anwani za Makazi kilichofanyika leo tarehe 08 Aprili 2022 jijini Dodoma.
Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Mhandisi Kundo Mathew (Mb) (aliyeketi katikati) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Wakaguzi wa Ndani wa Mikoa baada ya kufungua kikao kazi cha siku mbili cha kuandaa mpango kazi wa ukaguzi wa operesheni ya Anwani za Makazi kilichofanyika leo tarehe 08 Aprili 2022 jijini Dodoma. Aliyeketi Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Anthony Mtaka na kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya TEHAMA wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mulembwa Munaku
.............................................................................
NAIBU Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Mhandisi Kundo Mathew amewataka Wakaguzi wa Ndani wa Halmashauri zote nchini kusimamia vema utekelezaji wa operesheni ya Mfumo wa Anwani za Makazi inayoendelea kutekelezwa katika mikoa yote 31 nchi nzima.
Kauli hiyo ameitoa leo April 8,2022 jijini Dodoma wakati akifungua kikao kazi cha wakaguzi wa ndani wakuu wa mikoa Mhandisi Kundo amesema wakaguzi wa ndani wanatakiwa kusimamia matumizi mazuri ya fedha ambazo zimepelekwa katika mikoa na kushuka katika ngazi za halmashauri kutekeleza operesheni hiyo muhimu
“Sina shaka na weledi wenu isipokuwa Wizara imeitisha kikao hiki kwa lengo la kujadiliana, kupeana uzoefu na kupanga mikakati ya kufanya ukaguzi wa operesheni ya Anwani za Makazi kwa kuwa mnalo jukumu kubwa la kuhakikisha fedha zilizotolewa zinatumika kwa makusudi yaliyopangwa kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za fedha ili kuhakikisha malengo ya Serikali yanafikiwa”, amesisitiza Naibu Waziri huyo
Naibu Waziri Kundo amesema kikao hicho kinatoa fursa kwa wakaguzi wa ndani kuielewa operesheni hiyo, fedha zilizotolewa na namna zitakavyotumika ambapo wakaguzi wa ndani wa halmashauri zote nchini wanatakiwa kuwa sehemu ya utekelezaji wa eperesheni hiyo badala ya kusubiri kukagua nyaraka ofisini baada ya kukamilika kwa zoezi zima.
“Twendeni tukafanye kazi kuendana na kasi ya operesheni ili kuhakikisha fedha zilizopelekwa katika mikoa yote nchini kwa lengo la kutumika kutekeleza operesheni hiyo, ambazo ni shilingi bilioni 27.3 kwa Mikoa 26 ya Tanzania Bara na milioni 622 kwa mikoa mitano ya Zanzibar zinasimamiwa kwa weledi mkubwa” amesema Mhandisi Kundo
Ameongeza kuwa mfumo huo ulikuwa utekelezwe kwa miaka mitano lakini kwa sasa unatekelezwa kwa miezi mitano, hivyo wanahitajika watu makini watakaochukua hatua madhubuti ili kuhakikisha mianya yote ya kukwamisha utekelezaji kwa kiwango kinachohitajika kwa kigezo cha udharura inazibwa na malengo ya operesheni hiyo yanatimia.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mkurugenzi wa TEHAMA wa Wizara hiyo, Mulembwa Munaku amesema kuwa ni suala la msingi na pia ni wajibu wa wakaguzi wa ndani kukagua matumizi ya fedha za umma na Wizara hiyo kupitia ofisi ya Katibu Mkuu ipo tayari kuweza kutoa ushirikiano na kuhakikisha kwamba mpango kazi utakaoandaliwa katika kikao kazi hicho unatekelezwa kwa ukamilifu
Naye Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Anthony Mtaka amesema kuwa kikao hicho ni msingi mzuri kwa wakaguzi wa ndani wakiwemo wa Mkoa anaousimamia kufanya ukaguzi wa fedha zitakazotumika katika operesheni hiyo
Akizungumza katika kikao kazi hicho, Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Wizara hiyo, CPA, Joyce Christopher amesema kuwa wakaguzi wa ndani wanalo jukumu la kutoa hakikisho la mifumo iliyowekwa na Serikali namna inavyofanya kazi, kushiriki katika utekelezaji ili kuhakikisha malengo ambayo yamepangwa yanafikiwa kama ilivyotarajiwa.