Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka akiongea na waandishi wa habari Ofisini kwake leo Jijini Dodoma kuhusu maadhimisho ya Mei Mosi ambayo kitaifa yatafanyika mkoani Dodoma.
Rais wa shirikisho la Vyama vya wafanyakazi (TUCTA)Tumaini Nyamhokya akiongea kuhusu mipango ya maadhimisho ya siku ya wafanyakazi-Mei Mosi ambapo amewataka wafanyakazi kuhudhuria wa wingi na kuelimishana umuhimu wa sensa ya watu na makazi.
RAIS wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye kilele cha siku ya wafanyakazi-Mei Mosi itakayofanyika Kitaifa jijini Dodoma.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka ameeleza hayo leo wakati akiongea na vyombo vya habari kuhusu Mkoa wa Dodoma kuwa mwenyeji wa maadhimisho ya sherehe za Mei Mosi kitaifa,2022 huku akiwataka wakaazi wa mkoa huu kutumia tukio hilo kama fursa kibiashara.
"Mkoa wetu umepewa heshima ya kuwa mwenyeji wa sherehe za Mei Mosi kitaifa ,sherehe hii itaambatana na matukio na shughuli mbalimbali katika juma la maadhimisho kabla ya kilele hivyo niwaombe wafanyabiashara kujiandaa kuwahudumia zaidi ya watu 3000 ambao watahitaji huduma za kijamii kama vile malazi ,chakula,mavazi na nyinginezo",amesema Mtaka.
Ameeleza kuwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma inashirikiana kwa ukaribu na shirikishio la wafanyakazi (TUCTA),Chama kinachoratibu maadhimisho ya 2022 TALGWU,Ofisi ya Waziri Mkuu_Kazi na wadau wengine wa maendeleo nchini. Akielezea fursa zitakazopatikana kupitia maadhimisho hayo,
Mtaka amesema katika kufikia azma ya Serikali ya kuhakikisha kila fursa inayojitokeza inachangia ujenzi wa uchumi imara,Ofisi yake kwa kushirikiana na wadau imeazimia kutumia fursa hiyo kuziunganisha sekta zote za kiuchumi kwa manufaa ya taifa.
"Tumepanga kuandaa maadhimisho ya kipekee ,kwani maadhimisho haya ni ya pili kwa Rais Samia tangu awepo madarakani", amesema Mkuu huyo wa mkoa wa Dodoma.
Pamoja na hayo Mtaka amezitaja shughuli mbalimbali kuelekea kilele cha maadhimisho ya Mei Mosi kuwa ni pamoja na kikao cha wahariri na uzinduzi wa hashtag,michezo mbalimbali ikihusisha Drafti,riadha,mpira wa miguu,mpira wa Pete,kuvuta kamba,kufukuza kuku na bao.
"Michezo hii itafanyika kwenye viwanja vya Jamhuri,Kilimani Veteran,St John University,sheli wajenzi,Chinangali park,Vijana na mtekelezo -Dodoma Central", amefafanua Mtaka.
Mkuu huyo wa mkoa wa Dodoma amesema maonyesho mbalimbali ya Mei Mosi yakiambatana na maonyesho ya OSHA yatafanyika katika ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Center kuanzia tarehe 22 Aprili hadi 30 Aprili 2022 ambayo yatashirikisha makundi mbalimbali yakiwemo Viwanda,Wizara ,Vyama vya wafanyakazi na taasisi za fedha.
Mengine ni wafanyabiashara wa kati na wakubwa,Taasisi za Umma na za huduma, wajasiriamali wadogo na wa kati pamoja na wadau wengine wa maendeleo Kwa kuhusisha upimaji wa VVU,uchangiaji damu pamoja na utoaji wa chanjo ya UVICO-19.
"Kutakuwa pia na kongamano la midahalo kupitia vyombo vya habari na Katika na Katika kumbi za mikutano ambapo mada mbalimbali zitajadiliwa na Vyama vya wafanyakazi,waajiri na Serikali,kutunuku wafanyakazi hodari ngazi ya Mkoa ,kufanya ziara za utalii wa miradi ,burudani,maandamano ya wafanyakazi na zana za kazi,"amefafanua na kuongeza;
''Katika kuwakumbusha watanzania uzalendo tumeandaa kauli mbalimbali za Viongozi na nukuu zao ambazo watazisikiliza Katika maadhimisho ya Mei Mosi na zitakuwa zikitoka Kila Siku kupitia vyombo vya habari,niwaombe mpate fursa kusikiliza Ili mjifunze mengi kupitia hashtag yetu ya #MEIMOSI2022dodomakivingine,"amesema
Kwa upande wake rais wa TUCTA Tumaini Nyamhokya ametumia nafasi hiyo kuwataka wafanyakazi kuhudhuria kwa wakati maadhimisho hayo ili kutimiza malengo na kutaka sherehe hizo ziambatane na shughuli za maendeleo na watu.
"Nitumie nafasi hii kuwakumbusha wafanyakazi kushiriki kikamilifu akatika zoezi la sensa ya watu na makazi linalotarajiwa kuanza hivi karibuni, wafanyakazi pia mnapaswa kutumia fursa hii kuwashawishi watu wengine kuwa na utayari wa kuhesabiwa,"amesisitiza.