Naibu Waziri wa Fedha na mipango Hamad Hassan Chande akiongea kwenye uzinduzi wa baraza la Taifa la huduma jumuishi za fedha (WACFI) Jijini Dodoma ambapo ameeleza kuwa azma ya Serikali ni kupunguza utofauti ulipo katika upatikanaji na utumiaji wa huduma za fedha kati ya mwanamke na mwanaume utapungua kwa zaidi ya asilimia 9
Gavana wa Benki kuu ya Tanzania Prof. Florens Luoga akiongea kwenye uzinduzi wa baraza la Taifa la huduma jumuishi za fedha (WACFI)lenye lengo la kuwainua wanawake,uzinduzi huo umefanyika leo jijini Dodoma .
Na Dotto Kwilasa,Malunde 1 Blog-DODOMA
SERIKALI
kwa kushirikiana na sekta binafsi kupitia baraza la taifa la huduma
jumuishi za fedha imezindua rasmi kamati ya wanawake ya huduma jumuishi
za fedha (WACFI)yenye wajumbe 22 kutoka wizara mbalimbali za Serikali
,Taassi na Asasi za kiraia inayolenga kuongeza idadi ya wanawake katika
sekta ya fedha.
Akiongea
katika uzinduzi huo,Naibu Waziri wa fedha na mipango Hamad Hassan Chande
amesema hatua hiyo ni muendelezo wa utekelezaji wa mikakati ya Mpango
wa Pili wa huduma Jumuishi za Fedha unaolenga kujumuisha zaidi kundi la
wanawake katika matumizi ya huduma rasmi za fedha nchini.
Amesema,suala
la kuinua wanawake kiuchumi kwa kuongeza ushiriki wao katika sekta ya
fedha ni utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapindunzi ya mwaka 2020,
Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2021/22 -2025/26) na
Mpango Kabambe wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha wa mwaka 2020/21-2029/30.
"Kamati
hii ni muhimu na ina jukumu kubwa katika kubuni, kuchochea na kufuatilia
kwa karibu utekelezaji wa mikakati inayolenga kuongeza idadi ya
wanawake katika kuzifikia na kuzitumia huduma rasmi za fedha na hatimaye
kunyanyua kipato cha mwanamke;
Ni
matumaini yangu kuwa, baada ya uzinduzi wa leo mtahakikisha lengo la
Serikali la kupunguza utofauti ulipo katika upatikanaji na utumiaji wa
huduma za fedha kati ya mwanamke na mwanaume utapungua kwa zaidi ya
asilimia 90,"amesema Naibu Waziri huyo wa fedha.
Vilevile
amesisitiza kuwa azma ya kumnyanyua mwanamke kiuchumi ifanyiwe kazi
ipasavyo, kwa kushirikana na Kamati ya ushauri ya Kitaifa ya Utekelezaji
wa ahadi za Nchi kuhusu Kizazi chenye Usawa na kuongeza kuwa
utakapofanyika utafiti mwingine wa kisekta, baada ya utekelezaji wa
Mpango wa Pili wa Taifa wa Huduma Jumuishi za Fedha wa mwaka 2018-2022,
idadi ya watanzania watu wazima wanaotumia huduma rasmi za fedha itakuwa
imeongezeka mpaka asilimia 75 mwaka 2022.
"Ninategemea
kuona mbali na kutekeleza malengo mtakayokuwa mmejiwekea kupitia Kamati
hii yanayohusu masuala ya fedha, pia mtatekeleza mikakati yenye
kuhamasisha wadau wa huduma za fedha kutoa elimu ya masuala ya fedha kwa
wanawake hasa waishio vijijini ili waweze kunufaika na huduma na bidhaa
za fedha,"amesisitiza
Mbali
na hayo ameeleza kuwa elimu ya fedha ni muhimu ili kuwaondolea hofu
wanawake walio wengi katika kutumia huduma hizo ikiwemo mikopo na kwamba
bado kuna umuhimu wa kuwafundisha wanawake namna ya kusimamia mikopo na
kujitetea kisheria pale panapokuwa na uporaji wa fedha zao za mikopo
dhidi ya wenzi wao ili wasipate changamoto yakufanya marejesho.
"Kuna
umuhimu kwa wanawake kupewa elimu ya namna ya kuweka akiba, kufanya
uwekezaji, kukata bima na kujiandaa na maisha ya uzeeni,ipo haja ya
kuwahamasisha wadau wa sekta ya fedha kupendekeza mikakati itakayoongeza
upatikanaji wa takwimu za kijinsia hasa kutoka kwa sekta binafsi ili
zitusaidie kufanya maamuzi ya kisera kwa kuzingatia usawa wa
kijinsia,"amesema.
Kwa
upande wake Gavana wa Benki ya Tanzania,Prof. Florens Luoga amesema
Tanzania imekuwa ikitekeleza Mpango wa Pili wa Taifa wa Huduma Jumuishi
za Fedha (2018-2022), ambao unalenga kuongeza idadi ya watu wanaotumia
huduma rasmi za fedha kutoka asilimia 65 mwaka 2017 hadi asilimia 75
mwaka 2022.
Amesema
Mpango huo unatekelezwa kwa ushirikiano wa Serikali na sekta binafsi
kupitia Baraza la Taifa la Huduma Jumuishi za Fedha, ambalo lina wajumbe
22, kutoka Wizara mbalimbali za Serikali, taasisi na asasi zisizo za
Serikali.
"Mpango huu wa
Taifa unasisitiza kuongeza idadi ya wanawake inayofikiwa na kutumia
huduma rasmi za fedha, umeelekeza, kuundwa kwa Kamati ya Wanawake ili
kuratibu shughuli zote zinazohusu wanawake nchini katika Sekta ya Fedha
pamoja na kushauri njia bora ya kutatua changamoto zinazowakumba
wanawake katika kufikia na kutumia huduma rasmi za fedha,"amesema.
Ametaja
lengo la mpango huo kuwa ni kuhakikisha idadi kubwa ya wanawake
wanaofikiwa na kutumia huduma rasmi za fedha inaongezeka, kutoka
asilimia 61 mwaka 2017 hadi asilimia 73 mwaka 2022, pia kupunguza pengo
la uwiano wa kijinsia katika utumiaji wa huduma rasmi za fedha kati ya
wanawake na wanaume kwa asilimia 90.
"Kwa
mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, wanawake ni asilimia
51.3 ya watu wote nchini na asilimia 54 ya watu wenye umri wa miaka 60
na zaidi na asilimia 53.3 ya wafanyakazi wote wanaojishughulisha na
kilimo au biashara zisizo rasmi ni wanawake pia katika biashara,
asilimia 54 ya wamiliki wa biashara ndogo ndogo, na za kati (MSMEs)
nchini ni wanawake,
"Kwa
upande wa elimu, asilimia sita ya wanawake zaidi ya wanaume hawana elimu
rasmi, huku asilimia 67 ya wanawake dhidi ya asilimia 78 ya wanaume
ndiyo wanajua kusoma na kuandika lugha ya Kiswahili na kwa upande wa
lugha ya kiingereza ni asilimia 22 ya wanawake ikilinganishwa na
asilimia 31 ya wanaume ndio wanajua kusoma na kuandika,"ameeleza Gavana
Luoga.
Amesema kwa
kuzingatia takwimu hizo ni wazi kuwa wanawake wanakabiliwa na changamoto
kubwa katika kupata huduma za fedha na hii ni kutokana na kutokuwa na
elimu ya kutosha katika masuala ya fedha, mtazamo hasi kwa baadhi ya
jamii kuhusu wanawake pamoja na uwepo wa mila na tamaduni potofu
zinazosababisha mwanamke kutozifikia huduma rasmi za fedha.