Rais Mstaafu wa awamu ya Tatu nchini Kenya Mhe.Mwai Kibaki amefariki Dunia Leo Aprili 22, 2022 akiwa na umri wa miaka 90.
Rais wa Kenya Uhuru Kenyata ametangaza kifo cha Mwai Kibaki leo.
Kibaki alikuwa Rais wa tatu wa Kenya alihudumu kwenye kiti hicho kuanzia Desemba 2002 mpaka Aprili 2013.
Uhuru anamuomboleza mtangulizi wake kama kiongozi ambaye alileta ukuaji wa kiuchumi , demokrasia na kuimarisha hali ya uchumi ya Wakenya.
Uhuru anamkumbuka kwa jukumu lake la kupatikana kwa katiba mpya ya mwaka 2010 na kuongoza uidhinishaji wake.
Amesema kwamba bender azote katika majumba ya umma , wizara na balozi zote duniani zitasalia nusu mlingoti hadi pale atakapozikwa.
Na kufuatia tangazo la kifo chake viongozi mbali mbali nchini Kenya wameanza kutuma risala za rambirambi kwa famili ya Mwai Kibaki.
Kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga amesema kwamba 'alipata fursa ya kufanya kazi naye kama mbunge akiwa katika upande wa upinzani , kama waziri wa nguvu kazi na barabara katika serikali yake na baadaye kama waziri mkuu katika serikali ya muungano.
Raila Odinga: ''Asubuhi hii tumempoteza rais wa tatu wa Kenya, alikua mmoja wa wapigania uhuru wa nchi hii, ametumikia nchi hii kwa miaka mingi, kwa uwazi na utendaji kazi mzuri. Nilipata nafasi ya kufanya kazi na Mwai Kibaki, kwanza kama mbunge wa upinzani, pia kama mmoja wa mawaziri wake, na baadae kama waziri mkuu.''
Aliyekuwa wakati mmoja waziri wa fedha Musalia Mudavadi alichapisha ujumbe wake maombolezi katika twitter
Balozi wa Marekani nchini Kenya Eric Kneedler alihuzunishwa na kifo cha ghafla cha rais Mwai Kibaki . Alituma risala za rambirambi kwa jamii, Wakenya na rafiki wa mzee Kibaki wakati huu mgumu.