WANAFUNZI 80 WATORO WAMETAJWA KURUDI SHULE KATIKA WILAYA YA MULEBA KAGERA




************

Na Mbuke Shilagi Kagera.

Wanafunzi 80 ambao walikuwa watoro shuleni wamerudi shule katika halmashauri ya wilaya ya Muleba Mkoani Kagera, kwa kipindi cha mwaka 2020/2021 baada ya oparesheni iliyofanywa na viongozi wilayani humo.

Kauli hiyo imetolewa na Afisa elimu Msingi Mwl. Seveline Musyangi wakati alipotembelewa na mwandishi wa Habari wa Malunde Blog katika halmashauri hiyo akitaka kujua jinsi wanavyopambana kudhibiti utoro shuleni.

Musyangi amesema kuwa tayar wanafunzi hao waliokuwa watoro i wamesajiriwa kufanya mtihani wa kuhitimu darasa la saba mwaka huu, na kwamba wavulana ni 43 na wasichana 37.

Ametaja chanzo cha utoro kuwa ni umbali wa shule kwa wanafunzi, na kwamba utoro huo wa rejareja unasababisha wengi wao wasifanye mitihani ya kupanda darasa.

Ameongeza kuwa halmashauri hiyo imeendelea kufuatilia mahudhurio yao kila wiki toka wamesajiriwa kwa kushirikiana na walimu wakuu wa shule ili kuhakikisha wanafanya mtihani.

Ametoa wito kwa wazazi kuwa karibu na watoto wao ili kujua changamoto wanazopitia watoto wao kwa kuwasikiliza na kuwapa nafasi ya kuongea nao ili waweze kujua wanachowaza.

"Mtoto wako ni mtoto wetu, jamii nayo inayo nafasi ukiona mambo hayaendi vizuri kwa mtoto wako haendi shule, labda amebakwa au amefanyiwa ukatili wowote tushirikiane" amesema.

Kwa upande wake mzazi aliyejulikana kwa jina la Joseph Kamugisha ambaye ni baba wa watoto watano na mkazi wa Kata ya Katoke Kijiji cha Kimbugu, amesema kuwa changamoto inayosababisha utoro kwa wanafunzi, ufatiliaji wa wazazi kwa watoto wao ni mdogo hivyo unachangia watoto elimu kuichukulia kawaida, kiasi kwamba mtoto anaweza kuaga anakwenda shule kumbe yuko vichakani, na wakati mwingine watoto wa kike kuangukia kwenye mikono ya uharibifu.

Mzee Kamugisha ameongeza kuwa watoto wengi wanakimbilia kwenye uvuvi wakijidai kutafuta pesa na kuacha mambo ya msingi kama Elimu, na mambo mengi yanayohusu ndoto na malengo yao.

"Mimi Kama mzazi nitumie nafasi hii kuwaomba wazazi wenzangu kutoa ushirikiano wa karibu kwa watoto wetu, tusiwatelekeze tunapowapeleka shuleni, nasi tuhusike kwa karibu kufuatilia maendeleo yao ikiwa ni pamoja na kuwatembelea wawapo shuleni, ili kuzungumza na walimu wao na kujua maendeleo yao ya shule" amesema.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post