Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WATALII 900 KUTOKA NCHINI ISRAEL WANATARAJIWA KUTEMBELEA TANZANIA

Mwenyekiti wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Jaji Thomas Mihayo akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kwenye ofisi za TTB leo Jijini Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Jaji Thomas Mihayo (katikati) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kwenye ofisi za TTB leo Jijini Dar es Salaam

*********************

NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) inatarajia kuwapokea takribani watalii 900 toka Israel ambao watatembelea vivutio mbalimbali vya utalii nchini, wanatarajia kuja kwa makundi mawili, kundi la kwanza linatarajia kuwasili nchini Aprili 9,2022 na kundi la pili litawasili Aprili 16,2022.

Akizingumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Jaji Thomas Mihayo amesema ujio wa watalii hao ni kutokana na programu maalum ya Royal Tour ambapo mtandao maarufu wa habari nchini Marekani wa theGrio umetambua Juhudi za Rais Samia Suluhu katika kuiongoza vyema sekta ya Utalii nchini na kuifanya Tanzania kuwa kivutio cha kwanza cha Utalii Afrika 2022.

"Programu hii kwa ujumla imeanza kuleta matunda hasa kwa kuvutia watalii na wawekezaji mbalimbali kuja kutembelea katika nchi yetu na kuweza kuwa na ongezeko kubwa la watalii kwa hivi karibuni". Amesema Jaji Mihayo.

Amesema kuwa Wakala wa Utalii zaidi 30 kutoka katika nchi masokoya utalii yakiwemo Marekani,Ufaransa, Uingereza na Israel wamehamasika kutembelea nchini ili kujifunza na kujionea vivutio mbalimbali vya utalii kwa lengo la kuvitangaza katika nchi zao.

Aidha amesema kuwa wawekezaji kutoka Taifa la Bulgaria wanakusudiwa kuwekeza katika huduma za malazi za hadhi ya kimataifa kwa kujenga loji nne zenye hadhi ya nyota tano ambazo zitaendeshwa na kampuni ya Kempiski katika Hifadhi ya Ngorongoro hatua ambayo italeta matokeo chanya katika kuongeza idadi ya vyumba na wigo wa mnyororo wa huduma katika sekta ya utalii.

Pamoja na hayo Jaji Mihayo amesema idadi ya watalii kimataifa imeongezeka kwa asilimia 48.6% kutoka watalii 620,867 mwaka 2020 hadi watalii 922,692 mwaka 2021.

Ameeleza kuwa mapato yatokanayo na watalii wa kimataifa yanakadiriwa kuongezeka kutoka dola za Marekani Milioni 714.59 mwaka 2020 hadi dola za Marekani milioni 1,254.4 mwaka 2021 sawa na ongezeko la asilimia 76.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com