Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WATUMISHI SEKTA YA UVUVI WAFANYA KIKAO KUBORESHA UTENDAJI KAZI WAO


Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah akisaini kitabu cha wageni wakati alipofika kwenye Ofisi ya Katibu Tawala Mkoa wa Singida kabla ya kwenda kufungua kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Sekta ya Uvuvi kilichofanyika kwenye ukumbi wa Hoteli ya KBH.


Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah akifungua kikao cha Baraza la Wafanyakazi Sekta ya Uvuvi ambapo amewasihi watumishi wa sekta hiyo kufanya kazi kwa kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo ili sekta iweze kukua na kuchangia kwenye ongezeko la kipato cha wavuvi na pato la taifa kwa ujumla. Kikao hicho cha baraza la Watumishi kimefanyika kwenye ukumbi wa Hoteli ya KBH mkoani Singida.


Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji, Dkt. Nazael Madala akiwasilisha taarifa ya miradi ya maendeleo ya ukuzaji viumbe maji kwenye kikao cha baraza la wafanyakazi wa Sekta ya Uvuvi kilichofanyika kwenye Hoteli ya KBH mkoani Singida.


Mkurugenzi wa Idara ya Uvuvi, Bw. Emmanuel Bulayi akiwasilisha taarifa ya miradi ya maendeleo ya uvuvi kwenye kikao cha baraza la wafanyakazi wa Sekta ya Uvuvi kilichofanyika kwenye Hoteli ya KBH mkoani Singida.


Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah (katikati) akipokea Cheti cha shukrani kutoka kwa Mwenyekiti wa Klabu ya Michezo, Bw. Ally Suru (kulia) ikiwa ni ishara ya kutambua mchango wake katika kuendeleza na kuthamini shughuli za michezo. Kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Rasilimali Watu, Bw. Amosi Machilika.

..............................................

Watumishi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Sekta ya Uvuvi wamefanya kikao cha Baraza la Wafanyakazi kwa ajili ya kujadili namna walivyotekeleza bajeti ya mwaka 2021/2022 na kujipanga kutekeleza bajeti ya mwaka 2022/2023.

Kikao hicho kimefanyika Mkoani Singida ambapo Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Sekta ya Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah amewasihi watumishi kufanya kazi kwa kuzingatia weledi na kuona ni namna gani wanaweza kutatua changamoto zilizopo ili sekta hiyo iweze kuchangia zaidi kwenye pato la taifa.

Dkt. Tamatamah amesema kikao hicho ni muhimu kwa watumishi kwa kuwa watumishi wanashirikishwa kwa uwazi kuhusu namna walivyotekeleza bajeti ya mwaka 2021/2022 na kujipanga kutekeleza bajeti ya mwaka 2022/2023.

Aidha, amewasihi wajumbe wa walioshiriki baraza hilo kuhakikisha wanatoa ushauri mzuri ili kuhakikisha sekta ya uvuvi inakua na kuongeza mchango wake kwenye pato la taifa.

Pia, amewataka watumishi kuendelea kujilinda na magonjwa yanayoambukiza na yasiyoambukiza na kuwataka watumishi kufanya mazoezi ili kuendelea kuimarisha afya zao.

Katibu mkuu huyo amewapongeza wafanyakazi wa Sekta ya Uvuvi kwa kushiriki vyema kwenye mashindano ya (SHIMIWI), hivyo kuhakikisha wanaendelea kujiandaa ili katika mashindano yanayofuata wanafanya vizuri zaidi.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji, Dkt. Nazael Madala amesema kikao hicho kimewasaidia kujua changamoto walizokuwa wanakabiliana nazo katika utekelezaji wa bajeti na hivyo kuandaa mikakati ya kukabiliana nazo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi - Utumishi, Bi. Mary Mwangisa amesema kuwa watumishi wanapata elimu ya kuwasaidia kwenda kuboresha utendaji kazi wao kwa kuwa watakuwa wameshafahamu kazi zinazotakiwa kutekelezwa kulingana na bajeti iliyotengwa.

Akizungumza kwa niaba ya watumishi, Bi. Jane Kisanga amesema kuwa watumishi wamefarijika sana kushiriki kwenye kikao hicho ambacho kimewasaidia kuzitambua changamoto wanazokabiliana nazo na kujadili namna zinavyoweza kutatuliwa ili kuhakikisha sekta inaendelea kukua na kuchangia katika pato la taifa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com