Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAZIRI GWAJIMA AGUSWA NA PROGRAMU YA KIDIGITALI YA ICS KUTOA ELIMU YA MALEZI NA MAKUZI BORA KWA MTOTO

 


Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi maalum Dk. Dorothy Gwajima, akizungumza kwenye Shirika la ICS.

Na Marco Maduhu, SHINYANGA

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi maalum Dk. Dorothy Gwajima amelipongeza Shirika la Investing in Children and Strengthening their Societies (ICS), kwa kuanzisha programu ya malezi na makuzi bora ya mtoto kwa njia ya dijitali, inayolenga kukuza mahusiano chanya ya mtoto na mzazi.
Gwajima amebainisha hayo leo April 24, 2022 mkoani Shinyanga, wakati akipokea taarifa ya Programu ya malezi na makuzi bora ya mtoto kwa njia ya dijitali kutoka katika Shirika la ICS ambalo linajihusisha na shughuli za utetezi wa haki za watoto na wanawake mkoani humo.

Alisema sasa hivi kumekithiri kwa mmomonyoko wa maadili, sababu ya wazazi kuwa bize na maisha na kusahau malezi ya watoto wao, na kusababisha kuanza kufanyiana vitendo vya ukatili wenyewe kwa wenyewe hasa maeneo ya shule.

"Nimekuwa nikipokea meseji nyingi sana kuhusu watoto kufanyiana ukatili wao wenyewe mashuleni, wakienda huko msalani wanafanyiana vitu vya ajabu," amesema Gwajima.

"Naagiza maofisa ustawi wa jamii toeni elimu mashuleni kwa kushirikiana na walimu ya kupinga ukatili, sababu tumezoea kusikia watu wazima wakiwafanyia ukatili watoto, lakini sasa hivi watoto wameanza kufanyiana ukatili wao wenyewe sijui tunaelekea wapi,"ameongeza.

Aidha, amelipongeza Shirika hilo la ICS kwa kuanzisha Program hiyo ya malezi na makuzi bora ya mtoto kwa njia ya dijitali, ambayo ana imani itasaidia wazazi kufundisha watoto wao malezi bora na kupunguza matukio ya ukatili.

Naye Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko, amesema Program hiyo ambayo inatumika kwenye simu janja, itapunguza pia ubize wa wazazi kuchati vitu visivyo vya maana, bali watakuwa wakisoma stadi za malezi kwa njia ya kidijitali na kulea watoto wao vizuri na kuwa na maadili mema.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la ICS Kudely Sokoine, amesema wameanzisha program hiyo ili kufikia wazazi wengi, ambao watakuwa wakijifunza mara kwa mara stadi za malezi na kuboresha malezi ya watoto wao.

Alisema katika Programu hiyo kuna vipindi 12, ambavyo mzazi atakuwa akisoma kwa wiki kipindi kimoja, na malengo yao ni kufikia wazazi 6,000 lakini kwa sasa wameanza na wazazi 1,100.

"Nchini Tanzania program hii ya malezi na makuzi bora ya mtoto kwa njia ya dijitali Shirika la ICS kwa kushirikiana na NIMRI, chuo kikuu cha OXford, Cape Town Afrika kusini, kampuni ya IDEM na Shirika la Crown without Borders, tumeanza utekelezaji na kufanya majaribio ili kuona kwa namna gani tunaweza kufikisha elimu ya stadi za malezi na makuzi bora ya mtoto kwa wazazi na walezi kwa njia rahisi ya dijitali," amesema Sokoine.

"Mradi huu unakusudiwa kutekelezwa katika mkoa wa Mwanza na Shinyanga kwa kufikia wazazi 1,100 katika awamu ya kwanza na baadae kusambazwa katika mikoa mingine na kufikia wazazi zaidi ya 6,000 na mradi huu utaishauri Serikali katika mipango ya taifa ya afua za malezi na makuzi bora ili kupunguza vitendo vya ukatili," ameongeza.

Naye Meneja miradi wa Shirika hilo la ICS Sabrina Majikata, amesema program hiyo ParentAPP ni tolea la program iliyoundwa kwa ajili ya kufikisha elimu ya malezi na makuzi bora ya mtoto kwa wazazi na walezi walio na vijana wenye kuanzia umri wa miaka 10-17, program ambayo imeundwa kuwezesha wazazi kujifunza bila kutumia mtandao (Offline) kwa kutumia simu janja katika maeneo yote ikiwamo mashambani.

Anasema program hiyo inampa mzazi au mlezi fursa ya kujifunza maudhui wakati wote, anapokuwa na nafasi kwa kupata maarifa na stadi za kukabiliana na changamoto za malezi ya watoto.

Nao baadhi ya wazazi mkoani Shinyanga ambao ni wanufaika wa program hiyo akiwamo Mwajuma Msabila, amesema imekuwa na msaada mkubwa sana katika kuhakikisha wanawalea watoto wao katika malezi bora na maadili mazuri, kwa kupata elimu ya stadi za malezi.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi maalum Dk. Dorothy Gwajima (kulia), akiwa na Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko katika Shirika la ICS.

 Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi maalum Dk. Dorothy Gwajima akizungumza katika Shirika la ICS.

 

Mkuu wa wilya ya Shinyanga Jasinta Mboneko, akizungumza kwenye Shirika hilo la ICS.

 

Afisa maendeleo ya jamii mkoani Shinyanga Tedson Ngwale, akizungumza katika Shirika hilo la ICS na kupongeza kazi kubwa ambayo wanaifanya na kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa mipango yake mbalimbali ya utetezi wa haki za mtoto na wanawake.

Mkurugenzi wa Shirika la ICS Kudely Sokoine, akielezea Program ya malezi na makuzi bora ya mtoto kwa njia ya dijitali kwa Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi maalum Dk. Dorothy Gwajima (kulia) na kuisikiliza Programu hiyo kwa makini.

 

Mzazi Mwajuma Msabila, akielezea namna wanavyonufaika na Programu ya malezi na makuzi bora ya mtoto kwa njia ya dijitali.

Meneja miradi kutoka Shirika la ICS Sabrina Majikata, akimuelezea Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi maalum Dk. Dorothy Gwajima namna ya kujiunga na ParentAPP kwa kutumia Playstore na kupata Programu za malezi na makuzi bora ya mtoto kwa njia ya dijitali.

Maafisa wakiendelea kujiunga na Programu hiyo.

Maofisa ustawi wa jamii, maendeleo na katibu wa Waziri (kushoto) wakiwa katika Shirika la ICS wakifuatilia Programu ya malezi na makuzi bora ya mtoto kwa njia ya dijitali.

Na Marco Maduhu, SHINYANGA.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com