**************************
Wizara ya Maliasili na Utalii imesema itaendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kupitia ofisi za upelelezi za mikoa na wilaya katika kushughulikia masuala yote yanayohusu uhalifu wa wanyampori na mazao ya Misitu.
Kauli hiyo imetolewa leo mkoani Singida na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Juma Mkomi wakati akifungua kikao kazi cha Wizara kilichowahusisha Wakuu wa Upelelezi wa Mikoa [RCO], Makamishina wa Uhifadhi, na Wakuu wa Kanda wa Jeshi la Uhifadhi wa Wanyamapori na Misitu (JU).
‘’Ni matumani yangu mtatumia mjumuiko huu vizuri ili ninyi wenzetu muweze kutusaidia namna bora ya kuwezesha kuliimarisha Jeshi letu pamoja na kukuza ushirikiano baina ya Jeshi la Uhifadhi na Jeshi la Polisi.’’ amesema.
Aidha, amesema kuwa Wizara katika kutekeleza jukumu lake la uhifadhi wa rasimali za Wanyamapori na Misitu ikiwa katika mfumo wa kiraia ilikutana na changamoto mbalimbali hali iliyoilazimu kubadili Mfumo wa utendaji kazi wa Taasisi 4 za Uhifadhi ambazo ni Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro [NCAA, Shirika la Hifadhi (TANAPA), Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kuingia rasmi kwenye mfumo wa kijeshi.
Naibu Katibu Mkuu Juma Mkomi amezitaja baadhi ya changamoto zilizokuwepo kuwa ni pamoja ba ugumu wa upatikanaji wa vitendea kazi, Ujangili wa kutumia silaha za kivita na ucheleweshwaji wa ushughulikiaji wa mashauri ya kinidhamu kwa watumishi na kukosekana kwa mnyororo wa utoaji Amri.
Mbali na hilo, Mkomi amelipongeza Jeshi la Polisi kwa namna ambavyo limekuwa likishirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii katika kupambana na ujangili wa Wanyamapori na Mazao ya Misitu kabla na baada ya kuanzishwa kwa Jeshi la Uhifadhi.
‘’Wizara imeendelea kuwajengea uwezo Maafisa na Askari kwa kuwapelekea kozi mbalimbali hususan kozi za ukusanyaji taarifa,uchunguzi pamoja na Uendeshaji wa Mashitaka; mpaka sasa idadi ya maafisa na askari ambao wameshapata mafunzo bado ni ndogo ikilinganishwa na ukubwa wa maeneo ya kiutendaji. Amebainisha.
Ameeleza kuwa Jeshi la Polisi kupitia Ofisi za Maafisa upelelezi wa Mikoa na Wilaya limeendelea kuwa msaada mkubwa katika Nyanja hizo.
Hata hivyo, ameongeza kuwa lengo la kikao hicho ni kulitambulisha Jeshi la Uhifadhi Wanyapori na Misitu na kuomba ushirikiano kwa Watumishi wa Jeshi la Uhifadhi pindi wanapo tekeleza majukumu yao
Naye Mratibu wa Jeshi la Uhifadhi wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Fidelis Kapalata amesema Kikao kazi hicho cha Wizara na Wakuu wa Upelelezi Mikoa (RCO) kitadumisha ushirikiano baina ya Jeshi la Uhifadhi na Jeshi la Polisi kupitia upelelezi na hivyo kuimarisha utendaji kazi wa Jeshi hilo.