Na Agness Nyamaru,Arusha.
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amewataka wanahabari kutumia kalamu zao kukabiliana na changamoto zilizopo nchini na barani Afrika juu ya rasilimali zinazoharibiwa ili tatizo liweze kutatuliwa.
Ameyasema hayo leo wakati akizindua maonyesho kuelekea Kilele cha Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari duniani, Mei 5 mwaka huu ambapo mgeni rasmi katika kilele hicho anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ikiwa kauli mbiu ya yake ni "Uandishi wa habari na changamoto za kidigiti" ambapo alisema wajibu wa sekta ya habari ni kusaidia bara la Afrika, rasilimali zilizopo zibadilike kuwa baraka kwa watu wake ili kuona matokeo ya rasilimali hizo.
Alisema wakati umefika kwa wanahabari kuchukua maamuzi ya kusaidia bara hilo kufaidika na rasilimali zake na watu wake wajivunie kuwa waafrika na wajivunie kuwa kwenye bara lenye rasilimali za kutosha.
"Tukipewa hesabu ya rasilimali tulizonazo na ukilinganisha na mabara mengine hatupaswi kuwa hapa tulipo lakini kila mmoja wetu anapaswa kutimiza wajibu wake na wanahabari tunalo jukumu hilo kubwa la kubadilisha mambo maana hayapo sawa", alisema Nnauye.
"Angalia maovu mengi yaliyopo kwenye bara la Afrika sehemu ambapo kuna rasilimali nyingi ndipo watu wanapogombana zaidi, na sehemu ambapo kuna rasilimali za kutosha ndipo watu wake wanapoteseka sana sasa umefika wakati wa waandishi kusimama kusaidia kubadilisha mambo hayo, "alisisitiza Waziri huyo.
Aliongeza kuwa Serikali ina wajibu wa kutekeleza mazingira mazuri ikiwa kwa sasa maendeleo mazuri ya Sayansi na teknolojia ni vyema kuwe na uwezekano wa kaona namna ambavyo tasnia ya habari inasaidia jamii kwa kuona fursa kwenye mabadiliko hayo.
Alisema kutokana na siku hiyo ya uhuru wa vyombo vya habari na kuwasilishwa kwa mada tofauti tofauti wanahabari watapata uelewa juu ya Sheria mbalimbali zinazogusa sekta hiyo nchini,mijadala na uelewa wa Sheria mbalimbali zinazogusa tasnia ya habari hasa sheria za huduma za habari ya mwaka 2016 pamoja na kanuni zake.
"Hapa nchini kwetu sheria zinatungwa na bunge nichukue nafasi hii kumpongeza Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr Tulia Aksoni kwa utayali wake alionieleza kuwa wanasubiri tukamilishe... leteni tufanye mabadiliko ili tasnia ya habari iende kwa kasi, hivyo bunge lipo tayari sisi tukamilishe kwani bunge letu lina kazi ya kutunga na kufuta sheria zinazo kwaza ukuaji wa sekta mbalimbali, "alisema Waziri huyo.
Alisema anatumaini waandishi hao watatumia fursa nyingi katika kujadili na kutafuta njia bora za kushughulikia na kukabiliana na changamoto zinazowakumba huku wakiainisha fursa zilizopo katika kuendeleza sekta ya habari barani Afrika.
Naye Katibu Mkuu wa wizara hiyo Jimmy Yunaz alisema kupitia mkutano huo sekta ya habari inaendelea kuchangia ukuaji wa uchumi na kuchagiza uhuru wa Vyombo vya habari Duniani.
"Sekta ya habari inaendelea kuchangia vyema katika ukuaji wa uchumi wa nchi na pato la taifa kupitia mitandao ya kijamii," alisema
Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) ,Rose Reuben alisema uandishi wa habari ni jambo linalogusa jamii na kuleta maendeleo katika jamii na nchi kwa ujumla.
Alisema kwa sasa wapo kuangalia ukuaji wa teknolojia unavyokuwa kwa kasi,huku wakiangalia changamoto zinazowakumba waandishi wa kike katika kazi zao na kuzifanyia kazi.
Mkurugenzi huyo alisema kwa sasa wanapaswa kubadilika maana uandishi wa zamani umepitwa na wakati na wanapaswa kuandika habari kwa ajili ya mabadiliko ya taaluma yao wenyewe,jamii,na nchi kwa ujumla.
Kwa upande wake Mkurugenzi mtendaji umoja wa vyama vya waandishi wa habari Tanzania (UTPC) Abubakar Harssan alisema dunia imebadilika na vitu vingi vimehamia kwenye mitandao ya kijamii hivyo amewataka waandishi wote kutumia vyema mitandao hiyo ili kufanya jamii ikawa na uelewa mpana wa kile kinachoendelea na kuweza kupata mambo muhimu ya kihabari.
Social Plugin