Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

DC NGUVILA : TUACHE UPANDISHAJI HOLELA WA BEI ZA BIDHAA KWA KISINGIZIO CHA ONGEZEKO LA BEI YA MAFUTA


Mkuu wa Wilaya ya Muleba Mh. Toba Nguvila akizungumza
Mkurugenzi Mtendaji wa Halimashauri ya Wilaya ya Muleba Ndg. Elias Kayandabila
Khalfan Abubakari Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wilaya ya Muleba
Greyson Mwengu Katibu tawala Wilaya ya Muleba
Kushoto ni Mkuu wa Wilaya Mhe. Toba Nguvila, katikati ni Mkurugenzi Mtendaji Elias Kayandabila na kulia ni Afisa Biashara Dickson Mnyaga


*****

Na Mbuke Shilagi Kagera.

Mkuu wa Wilaya ya Muleba Mhe. Toba Nguvila amewataka wafanyabiashara wa Wilaya ya Muleba kuacha kupandisha bei kwa bidhaa zinazopatikana ndani ya wilaya ya Muleba kwa kisingizio cha ongezeko la bei ya mafuta.


Akizungumza katika mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba Mei 7,2022 ulio wahusisha viongozi wa Wilaya na Wafanyabiashara, Mhe. Nguvila amewasihi wafanyabiashara kuwajali wateja wao ili waweze kupata faida ambayo ni halali bila kuwaumiza wananchi kwa kuwauzia bidhaa kwa bei ya juu.


"Tukizingatia hayo tutakuwa na wateja wengi, mtafanya mzunguko wa biashara kuwa mkubwa na mtapata faida kubwa. Hata upendo kwenye jamii utakuwa mzuri mkiuza bidhaa zenu kwa wananchi kwa bei ambayo ni nzuri." ameeleza Mhe. Nguvila.


Aidha, amewashauri wafanyabiashara kuwa kadri wanavyoagiza mzigo mara kwa mara na kuuza kwa bei nafuu watakuwa kwenye nafasi ya kupata faida zaidi kuliko kuuza kwa bei kubwa na kusababisha bidhaa kukaa dukani muda mrefu bila kununuliwa.


Pia ameagiza kufanyika kwa mkutano wa Baraza la wafanyabiashara mara mbili kwa mwaka ili kujadili masuala mbalimbali yanayowahusu wafanyabiashara pamoja na wanufaika wa biashara ikiwa ni kukuza biashara na kutatua changamoto mbalimbali za wafanyabiashara.


Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Muleba Ndg. Elias Kayandabila amewasihi wafanyabiashara kuacha ubinafsi kwa kuwaeleza kuwa sio jambo jema kupandisha bei ya vitu vilivyomo kwenye maduka yao baada ya bei elekezi kutangazwa na Serikali.


Naye Katibu Tawala wa wilaya ya Muleba Ndg. Greyson Mwengu amewaomba wafanyabiashara kuweka bei ambazo haziwaumizi wananchi hasa kwa bidhaa zinazopatikana ndani ya wilaya kwa kuwaeleza kuwa wakiendelea kupandisha bei hasa za bidhaa za vyakula wanaweza kupelekea wananchi kushindwa kumudu gharama za bidhaa hizo na hatima yake bidhaa zao kutonunuliwa kabisa.


Afisa Biashara wa wilaya ya Muleba Ndugu Dickson Mnyaga amewaomba wafanyabiashara kupunguza bei, hasa kwa bidhaa kama mafuta ya kupikia, sabuni za kufulia bidhaa za ofisini kama karatasi nyeupe na vyakula kama nyama. Bidhaa hizi zishushwe bei na kuuzwa kwa bei stahili ambazo wananchi wanazimudu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com