Mwenyekiti wa Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA Taifa Mhe. Freeman Mbowe amewataka viongozi wa CHADEMA kuheshimu vyama vya siasa vingine huku akiwatahadharisha wale walio ndani au nje ya CHADEMA watakaoihujumu CHADEMA.
Mbowe ametoa kauli hiyo leo Mei 11, 2022 CHADEMA wakati akihutubia kikao cha Baraza Kuu katika Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam lililohudhuriwa na wajumbe zaidi ya 400 wa chama hicho wanaotoka katika mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara na Zanzibar.
Mbowe amewataka viongozi wa vyama vya siasa nchini kuacha tabia ya kurushiana maneno ya matusi na ya kuudhi kwenye mitandao au mikutano ya kisiasa huku akibainisha kuwa kutofautiana kwa mawazo miongoni mwa vyama vya siasa ndio ukuaji wa Demokrasia na haipaswi kuwa chanzo cha chuki
“Tusipoteze muda kujadili wengine, tutumie muda mwingi kujenga CHADEMA. Lazima tuheshimu vyama vingine vya siasa kwa sababu hujui kesho chama kipi kitakuwa chama kikuu cha upinzani. Tusiwe wepesi wa kushambulia wenzetu kwa sababu huwezi jua huenda uwezo wao umeishia hapo",amesema Mbowe.
"Chama chetu kinapaswa kuwa wanyenyekevu kwa vyama vingine vya siasa, kuheshimu maamuzi ya vyama vingine vya siasa, na chama hiki kifanye kazi ya kujenga harakati za kweli na sio kazi ya kutukana vyama vingine kwenye mitandao au kwenye mikutano.
"Ninaona kwenye mitandao maneno ya maudhi ambayo viongozi wangu mnafanya kudhalilisha vyama vingine, hii inatakiwa kuisha sasa, tuheshimu Vyama vya wenzetu tuheshimu mawazo yao, tunapotofautiana ndio Demokrasia yenyewe" ,amesema Mbowe
Aidha Mbowe ameeleza kuwa kutofautiana kwa ajenda baina ya CHADEMA na ACT Wazalendo kunapaswa kuheshimiwa na haina haja ya kuonana wabaya
"Wenzetu wa ACT wamekuwa na ajenda yao ya Tume huru, CHADEMA hatuna haki ya kuwaambia msitake Tume huru, wacha watake wanachotaka wao, tunatofautiana katika njia na hiyo ndiyo namna ya kujenga Demokrasia, sio kila mmoja anayepingana na CHADEMA basi ni mbaya, hapana".
"Kwanza niweke sawa, hatukatai tunahitaji Tume huru, kwahiyo ajenda ya ACT ni ajenda yeto wote, lakini Tume huru haipaswi kusimamisha mchakato wa Katiba, mchakato wa Katiba uendelee wakati wengine wanarekebisha sheria ambazo ni mbovu, haya mambo yaende kwa kutegemeana",amesema Mbowe.
"Wiki ijayo tutaanza vikao vya CHADEMA na CCM Tumepanga kukutana Delegation ya CHADEMA yenye wajumbe wasiozidi 10 na Delegation ya CCM wiki inayokuja, tutaenda kuzungumza nini kinafanya taifa letu lisiende mbele. Tunataka kutengeneza mahusiano ya msingi. Watu wetu wamekuwa na hofu kwa sababu ya kutoaminiana. Tunataka kujenga taifa",ameongeza Mbowe.
Aidha amezitaka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kuheshimu Demokrasia bora.
Social Plugin