Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

CHADEMA NA TAMKO JINGINE KUHUSU MDEE NA WENZAKE 18..SASA KUBAINI WASALITI

 

Waliokuwa wanachama wa Chadema, Halima Mdee na wenzake 18 
***
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimesema kesi ya madai iliyofunguliwa na wabunge viti maalumu 19 kupinga kufukuzwa ndani ya chama hicho kitawasaidia kuwatambua waliohusika na uteuzi wa wabunge hao kinyume na CHADEMA.


Akizungumza na wanahabari hii leo Makao Makuu ya Chama hicho jijini Dar es laam Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Bara, Benson Kigaila,amesema kwa kuwa kina Mdee wamekwenda mahakamani hivyo kupitia kesi hiyo watapata kuona vile vilivyokuwa vimejificha nyuma ya pazia.


“Kuna maswali kwamba hamtambui uchaguzi wa 2020, kwa nini mnalalamika kuhusu hawa wabunge. Tunalalamika kwa sababu kubwa mbili, ya kwanza wanatumia jina la Chadema kwamba iliwateua kuwa wabunge kitu ambacho si cha kweli. Kama wangekwenda tukaambiwa toka mwanzo wameteuliwa na CCM tusingelalamika. Lakini wakati ule tulikuwa hatujawafukuza,” amesema Kigaila.


Aidha Kigaila amesema Chadema kinalalamika kwa kuwa wabunge waliovuliwa uanachama wanabaki bungeni na kutumia fedha za umma bila uhalali.


“Wanatumia pesa za umma ambazo ni kodi zetu bila kuwa na uhalali, lakini cha tatu tunacholalamika ni kughushi nyaraka zilizofanya wateuliwe. Haya ndiyo mambo ambayo tunalalamikia. Sisi hatujalalamika kutaka hivyo viti,” amesema Kigaila


Kigaila ameongeza kuwa katika kikao cha Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe na Chama Cha Mapinduzi (CCM) pamoja na Rais Samia Suluhu Hassan, watakwenda kuzungumzia juu ya suala hilo.


Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mawasiliano, Itifaki na Mambo ya Nje Chadema, John Mrema, amesema wataitumia kesi hiyo kujua watu waliohusika kuwapeleka wanachama hao bungeni bila ya ridhaa ya chama chao.


“Tunakwenda kuwahoji nani alisaini barua zao na si ajabu kama nchi hii ingekuwa inafuata sheria watakuwa wana kesi ya jinai ya kughushi nyaraka za Serikali na kujipatia fedha sababu wamelipwa posho na mishahara kinyune na sheria,” amesema Mrema.


Pia ameiomba Mahakama Kuu kuwa kesi hiyo iendeshwe kwa dharura kwa kuwa ina maslahi kwa umma.


“Tunafikiri mahakama itachukulia kesi) serious, sababu ikikaa muda mrefu fedha za umma zitachezewa kinyume na katiba na si ajabu CAG akijakagua itakuwa eneo oa ukaguzi kuhoji mliwalipaje fedha za mishahara na posho mtu ambaye si halali,” amesema Mrema.


Mdee na wenzake 18, wamefungua kesi ya madai Na. 16/2022, katika Mahakama Kuu, Kanda ya Dar esSalaam, kupinga uamuzi wa Chadema kuwafukuza, ambapo wanaomba warejeshewe uanachama wao wakidai walivuliwa kinyume cha sheria.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com