Mkurugenzi mtendaji wa Shirika la Humuliza lililopo Wilayani Muleba Mkoani Kagera Bw. Victor Nestory
**
Na Mbuke Shilagi Kagera.
Shirika lisilo la kiserikali la Humuliza lililopo Wilayani Muleba Mkoani Kagera limewataka wazazi na walezi kuwaambia ukweli watoto wao juu ya mabadiliko katika jamii pamoja na utandawazi.
Akizungumza na Malunde 1 Blog Mkurugenzi wa Shirika hilo,Victor Nestory amesema kuwa mabadiliko ya utandawazi katika jamii yanaendana na mabadiliko ya mwili kwa watoto hivyo wazazi wanatakiwa kuwa wazi kwa watoto wao ili wajue kinachoendelea.
Nestory amesema kuwa jamii imezipuuza Mila na desturi kwa asilimia kubwa na kwamba watu wamekuwa bize na maisha na hata kama mtoto akidanganya juu ya jambo lolote mzazi anakuwa hajui.
"Wazazi wamewatupia mzigo mkubwa walimu kiasi kwamba na wao wanalemewa hivyo wazazi tubadilike tutumie nafasi zetu kuwaelimisha na kuwafatilia watoto wetu na sio kuwaachia waalimu tu", amesema Nestory.
Amewataka pia wazazi kuungana ili kuwasaidia watoto kupata chakula Mashuleni ili kuwaepushia na vishawishi wanavyokumbana navyo njiani kutokana na njaa.
Kwa upande wake Meneja miradi , Lighitiness Mpunga amesema kuwa watoto wapo katika mazingira hatari kuanzia njiani wanapo elekea mashuleni mpaka majumbani kwao.
"Watoto wapo katika mazingira hatarishi maana ndani unakuta kuna mjomba, baba mdogo, babu ambapo wote hao wamekuwa ni hatari kwa watoto wetu nao watoto wamekuwa wakimya sana kusema kama wamefanyiwa ukatiri hivyo wazazi wakae karibu nao na kuwaeleza tu ukweli", amesema.
Meneja huyo ameongeza kuwa wazazi wanatakiwa kuwa makini zaidi kwa watoto hasa wakati wanapopata wageni majumbani mwao kwa kuwalaza chumba kimoja watoto na wageni.
"Watoto wamekuwa wakiwindwa kila kona hivyo wazazi wanatakiwa kuwaweka wazi kabisa ili wajue nini ni kibaya kwao", amesema.