BOSI WA SHULE YA SUN ACADEMY MBARONI KWA TUHUMA YA KUMPIGA MZAZI ALIYETAKA UHAMISHO WA MTOTO WAKE


Kamanda wa polisi mkoani Iringa ACP Allan Bukumbi akionesha baadhi ya vitu ambavyo vimekamtwa kwenye uhalifu uliofanyika katika baadhi ya wananchi wa mkoa wa Iringa
Kamanda wa polisi mkoani Iringa ACP Allan Bukumbi akionesha baadhi ya vitu ambavyo vimekamtwa kwenye uhalifu uliofanyika katika baadhi ya wananchi wa mkoa wa Iringa na hilo gari lilitumika katika kufanya shughuli za utapeli kwa wananchi wa Iringa

Na Fredy Mgunda - Iringa.

MMILIKI wa shule ya Sun Academy mkoani Iringa Nguvu Chengula anashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani humo kwa tuhuma za kumshambulia na kumjeruhi kwa kutumia Kitako cha bastola mkazi wa manispaa ya Iringa Alifa Mkwawa baada ya kuibuka mzozo wa mtuhumiwa kugoma kutoa uhamisho wa mtoto wa mjeruhiwa.

Kwa mujibu wa Kamanda wa polisi mkoani Iringa ACP Allan Bukumbi akitoa taarifa ya matukio ya uhalifu kwa waandishi wa habari mkoani humo leo amesema tukio hilo limetokea mnamo Mei 16 mwaka huu majira ya saa sita mchana.

Amesema inadaiwa kuwa mjeruhiwa Alifa Mkwawa alifika katika ofisi ya Shule ya Sun Academy kwa lengo la kufuatilia uhamisho wa Mtoto wake anayesoma darasa pili shuleni hapo ambapo Mtuhumiwa aligoma kutoa uhamisho huo hali iliyozusha majibizano yaliyopelekea mtuhumiwa kutoa bastola na kufanya shambulizi hilo

ACP Bukumbi amesema kuwa licha ya mtuhumiwa kumiliki bastola hiyo kihalali aina ya Canik 55 yenye namba 6472-15100082, lakini ameitumia isivyo halali hivyo Jeshi la Polisi linaendelea kushikilia Mtuhumiwa huyo Nguvu Chengula akiwa na kielelezo cha bastola hiyo wakati likiendelea na upelelezi kabla ya kumfikisha mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili.

Amesema kuwa katika kupambana na kutokomeza matumizi na biashara haramu ya dawa za kulevya jeshi la polisi mkoa wa Iringa kwa nyakati tofauti maeneo ya vijiji vya Irambo na Ibumu kata ya Image wilaya ya Kilolo jeshi la polisi lilifanikiwa kukamata watuhumiwa watano na kuharibu mashamba ya bangi iliyolimwa kwa mchanganyiko wa mahindi na maharage.

ACP Bukumbi amesema watuhumiwa walitumia mbinu ya kulima vishamba vidogo mtawanyiko na kupanda bangi katikati ya mazao hayo kwenye maeneo ya misitu na makorongo ambapo mashamba hayo yanamilikiwa na Benjamin Mkapa Ngulo na shamba lingine linamilikiwa na Teso Wilbath ambao kwa ujumla mashamba yote yana ukubwa wa ekari mbili na nusu.

Amesema kuwa watumiwa wanane walikamatwa kwa kujihusisha na kilimo cha bangi na mtuhumiwa mmoja amekamatwa kwa kosa la kupatikana na bangi kilo mbili.

Katika hatua nyingine Kamanda wa polisi mkoani Iringa ACP Allan Bukumbi alisema kuwa jeshi hilo linamshikilia mwanamke mmoja anaitwa Desderia Mbwelwe mwenye umri wa miaka 56 kwa tuhuma za kulazimisha kufanya mapenzi na mtoto mwenye umri wa miaka nane (8) ambaye ni mwanafunzi wa darasa la tatu.

ACP Bukumbi amesema kuwa mwanamke huyo alifanikiwa kukamata mwanafunzi huyo kasha kumvutia kichakani na kumlazimisha kufanya mapenzi kwa kutumia nguvu kitendo kilichopelekea maumivu makali sehemu za siri za mtoto huyo na jeshi la polisi mkoa wa Iringa linamshikilia mtuhumiwa huyo na upelelezi ukikamilika litamfikisha mahakamani.

Katika hatua nyingine amesema jeshi la polisi mkoa wa Iringa linawashikilia watu watatu wakiwa na mabunda ya karatasi nyeusi zilizokatwa na kupangwa mfano wa pesa za kitanzania ambao walikuwa wamepanga kufanya utapeli mkoani humo wakitumia gari aina ya Mark x yenye rangi nyeupe namba za usajili ni T979 DWN inayomilikiwa na Herieth Khamis Mkazi wa Dar es salaam.

Amesema kuwa baada ya upekuzi waliwakuta na vipeperushi vya Sharif Majini, Pete za Bahati, Dawa aina ya IODINE, Vitamini B complex ambayo imechanganywa na maji na mara baada ya kufanya nao mahojiano walikiri kufika mkoa wa Iringa kwa lengo la kufanya Utapeli jambo ambalo halikufakiwa baada ya jeshi la polisi kuwakamata.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post