Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAZIRI GWAJIMA ALIPONGEZA SHIRIKA LA KIVULINI KUHAMASISHA UJENZI WA NYUMBA BORA MISUNGWI ....."TUPA NYASI WEKA BATI"



Waziri wa Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima  amelipongeza shirika la Kutetea Haki za Wanawake na Watoto la KIVULINI kwa jitihada za kuhamasisha ujenzi wa nyumba bora katika wilaya Misungwi mkoani Mwanza.

Akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha wa 2022/2023 Bungeni Mjini Dodoma leo , Dkt. Gwajima  amesema kuwa kampeni hiyo ya kuboresha makazi kwa wananchi wenye makazi duni imewezesha kujengwa kwa zaidi nyumba bora 5000 hadi kufikia mwezi Aprili mwaka huu.

“Kampeni hiyo ya ujenzi wa nyumba kwa gharama nafuu imekuwa ikifanyika kwa gharama ya kati ya shilingi milioni saba hadi kumi nyumba inasimama na nyumba hizi zimeongezeka kutoka 751 mwaka 2020/2021 hadi kufikia 5,002 Aprili mwaka huu 2022”, alisema Waziri Gwajima.

“Tunawashukuru sana shirika la KIVULINI kwa kutusaidia katika kampeni hii inayowezesha wananchi wenye makazi duni kutumia mifumo ya asili katika kusaidiana kujenga nyumba bora za makazi”, aliongeza Waziri Gwajima.

Waziri Gwajima pia amepongeza mchango unaotolewa na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali likiwemo shirika la KIVULINI katika mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto.

Shirika la KIVULINI katika kampeni hiyo imekuwa ikitumia kauli mbiu ya TUPA NYASI WEKA BATI kwa ajili ya kuhamasisha wananchi wa wilayani Misungwi kuondoa nyumba za nyasi na kujenga nyumba za mabati.

Vikundi 87 vya akinamama vya kusaidiana kujengeana nyumba bora za makazi tayari vimeundwa katika maeneo mbalimbali ya wilaya Misungwi.

“Wanachama wa vikundi hivi wanachangiana vifaa vya ujenzi vinavyotumika kujenga nyumba hizi za gharama nafuu,utaratibu huu umewezesha wananchi wengi kupata makazi bora”, alisema Yassin Ally Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la KIVULINI.

Akizungumzia hatua ya Waziri Gwajima kutambua mchango wa shirika hilo katika kuboresha makazi,Yassin amesema kuwa hatua hiyo ya serikali imewapa ari ya kuendelea kuhamasisha Jamii kujenga nyumba bora za makazi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com