KWAYA YA MT. KIZITO ZIARANI NCHINI KENYA


Kwaya ya Mtakatifu Kizito, Parokia ya Mwenyeheri Anuarite Makuburi, Jimbo kuu Katoliki la Dar es Salaam, inatarajia kufanya ziara ya kitume nchini Kenya kuanzia Mei 31 hadi June 6 mwaka huu.

Wakati wa ziara hiyo pamoja na mambo mengine, kwaya itashiriki kwenye misa maalum iliyoandaliwa na Jimbo Kuu la Nairobi, kuomba amani wakati na baada ya uchaguzi Mkuu wa nchi hiyo, utakaofanyika mwezi wa 8 mwaka huu.


Mbali na misa hiyo itakayoadhimishwa June 4, Kwaya ya Mt Kizito itakuwa na tamasha kubwa siku inayofuata ya June 5, tamasha litakalofanyika katika parokia ya Queen of Apostles Ruaraka, linalojulikana kama Kmk Gala.


"Tunakwenda kuhubiri amani, amani ya Wakenya ni amani ya Watanzania, na mbali ya kusali nao, Wakenya wawe tayari kupata burudani safi toka kwetu" alisema Nicetas Lyamuya, Mwenyekiti wa Kwaya ya Mt. Kizito.


Akiongea kuhusu ziara hiyo, Mkurugenzi wa Liturjia wa Jimbo Kuu la Nairobi, Padre Bernard Kabiu alisema "Tunawaomba wanakwaya, mapadre, walei na wote wenye mapenzi mema wafike katika matukio yote watakayofanya wanakwaya hawa ili wajifunze mambo mengi mazuri toka kwaya hii maarufu na bora kabisa katika ukanda huu wa AMECEA na kwingineko".


Misa ya kuomba amani itakayoanza saa tatu asubuhi, itaadhimishwa katika Kanisa la St Mathias Mulumba, na inatarajiwa kuongozwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Nairobi, Mhashamu Phillip Anyolo.


Pamoja na kushiriki matukio hayo makubwa mawili, pia kwaya ya Mtakatifu Kizito itafanya ziara katika parokia mbalimbali za Jimbo la Nairobi, Ngong na Machakos.


Kwaya ya Mtakatifu Kizito Makuburi, iliyoanza utume wake mwaka 1988, inaundwa na wanakwaya 120. Inatarajia kurudi nchini June 6 mwaka huu.


Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano cha Kwaya ya Mtakatifu Kizito Makuburi


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post