Mkuu wa Mkoa wa Simiyu David Kafulila (mwenye Suti ya bluu) akikagua Chujio la Maji kwenye bwawa la Maji Nkoma-Itilima.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu David Kafulila (kushoto) akiongea na mwenyekiti wa kijiji cha Mwamwita Matume Luhela pamoja na wananchi wa kijiji hicho mara baada ya kukagua mradi wa maji wa kijiji hicho.
Na COSTANTINE MATHIAS, Itilima.
MKUU wa Mkoa wa Simiyu David Kafulila amewataka wananchi wa Kijiji cha Mwamwita na Nkoma wilayani Itilima, kuhakikisha wanaitunza miradi ya maji ili iweze kuwanufaisha na kufikia malengo ya serikali.
Kafulila amesema bidhaa ya maji ni bidhaa muhimu na adimu ambayo kila mtu anaihitaji, ambapo lengo la serikali kufikia 2025 maji vijijini yafike kwa asilimia 85.
Mkuu huyo wa Mkoa ameyasema hayo jana, mara baada ya kutembelea mradi wa Maji kijiji cha Mwamwita pamoja na chanzo cha mradi huo ambao ni bwala la maji lililopo kijiji cha Nkoma.
Kafulila amesema malengo ya serikali ni kuona wananchi wanapata maji ambapo hadi sasa kuna kasi kubwa ya usambazaji wa maji ndani ya mkoa wa Simiyu kupitia fedha za Uviko 19 pamoja na miradi ya lipa kwa matokeo (P4R).
"Fedha za Uviko 19 zimeletwa kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji shilingi bil 2.8, miradi ya lipa kwa matokeo (P4R) zimeletwa bilioni 22 na zipo kwenye miradi ya maji’’ ,amesema Kafulila.
Ameongeza kuwa "Mradi wa Ziwa Victoria utatekelezwa katika vijiji 240 vya Mkoa wa Simiyu kwa bomba lenye urefu wa kilometa 190 ili kumaliza tatizo la uhaba wa maji ndani ya mkoa…zaidi ya bil 400 zinakuja katika mkoa mmoja kwenye maji’’.
Amesema katika bajeti ya 2022/23 katika wilaya ya Itilima miradi 8 ya maji itatekelezwa wakati huo 2021/22 pia ilitekelezwa miradi mingine minane ya maji na kufanya jumla ya miradi 16 ndani ya miaka miwili.
Awali Mwenyekiti wa Kijiji cha Mwamwita Matume Luhela ameishukuru serikali kwa kutekeleza miradi ya maji vijijini, huku akiiomba RUWASA kuendelea kupanua na kuongeza vituo vya kuchotea maji ili wafikiwe wananchi wengi zaidi.
"Lengo la serikali ni kuwafikishia wananchi Maji, tunaishukuru serikali kwa kutekeleza miradi ya maji lakini tunaomba vituo viongezwe ili kuwafikia wananchi wengi zaidi",amesema Mwenyekiti huyo.
Social Plugin