Mwanamke mmoja nchini Nigeria amefikisha baba mkwe wake kortini kwa madai ya kukataa aolewe na mwanawe.
Halima Yunusa alimshtaki baba mkwe wake katika Mahakama ya Kiislamu ya jimbo la Kaduna nchini Nigeria kwa kumzuia mwanawe Bashir Yusuf asimuoe.
Kwa mujibu wa taarifa ya gazeti la The Daily Trust, Halima aliiambia mahakama hiyo kuwa anapendana na mpenzi wake lakini baba yake Yusuf amekataa asimuoe.
Baba yake Halima aliiambia mahakama hiyo kuwa anafahamu kuhusu uhusiano wa mapenzi baina ya binti yake na Yusuf, lakini alikuwa hajatimiza vigezo vya kuoa.
Mzee Ibrahim alisema kuwa alimtuma Yusuf awalete wazazi wake ili kutimiza vigezo vya ndoa lakini hakurejea tena.
Yusuf alijitokeza tena baada ya mwaka mmoja na kumchukua Halima kisha walitoweka kwa siku tatu bila kurudi nyumbani na baadaye wazazi wake Halima waliambiwa walikuwa wameenda kwa shangazi yao.
Kulingana na mzee huyo, wawili hao walipelekwa katika kituo cha polisi ambako walikamatwa na kupatikana na hatia na baadaye wakaachiliwa kutoka kwenye kituo cha polisi na kutoroka hadi katika mji wa Abuja.
Lakini baadayeMzee Ibrahim alipokutana na baba yake Yusuf, alimuonya kuwa hatamruhusu Yusuf amuoe binti yake.
Baada ya kusikia hoja zao, korti hiyo alimuamrisha baba yake Yusuf kumruhusu kijana wake amuoe Halima la sivyo hmahakama itawafungisha ndoa.