Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

NDUGU AKODISHA WATU WATATU KWA SH. ELFU 50 NA KUMUUA KAKA YAKE


Kaimu kamanda wa jeshi la polisi Mkoa wa Kagera ACP Maketi Msangi

Na Mbuke Shilagi Kagera.

Jeshi la Polisi mkoa wa Kagera linamshikilia Dominic Petro (48) na wenzake watatu kwa tuhuma za mauaji ya kaka yake Pancras Petro (62) mkazi wa Kanyankombo Kijiji Cha Nyabishenge Kata Kaisho Wilaya ya Kyerwa Mkoani Kagera.


Akizungumza na vyombo vya Habari Kaimu kamanda wa Jeshi la polisi Mkoa wa Kagera ACP Maketi Msangi amesema kuwa watuhumiwa hao wametenda tukio hilo mnamo tarehe 20 Mei 2022 na kwamba Dominic Petro (48) ambaye ni mdogo wa marehemu aliwakodi wenzake watatu kwenda kumsaidia kufanya tukio hilo kwa makubaliano ya kuwalipa shilingi Elfu 50 ikiwa chanzo cha tukio hilo ni mgogoro wa ardhi (shamba).


Watuhumiwa hao wamejulikana kwa majina ya Isack Mujuni (26), Mnyambo mkazi wa Ibale, Nelson Ladslaus (26) mkazi wa Rwengoha, Nelson Michael (27) mkazi wa Ibale pamoja na Dominic Petro (48) mkazi wa Rwengoha ambaye ni mdogo wake marehemu.


ACP Msangi amesema kuwa watuhumiwa hao mara baada ya kufanya tukio hilo walikimbia kusikojulikana na kwamba jeshi la polisi lilianza msako mkali la kuwatafuta na mnamo tarehe 25 Mei 2022, watuhumiwa walikamatwa na baada ya kufanyiwa mahojiano ya awali watuhumiwa hao walikiri kufanya tukio hilo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com