Muonekano wa ofisi ya Mwenyekiti wa Kitongoji Namba 2 kijiji cha Nyaligongo kata ya Mwakitolyo wilaya ya Shinyanga na vitu mbalimbali baada ya kuharibiwa na wananchi wenye hasira kali
Muonekano wa ofisi ya Mwenyekiti wa Kitongoji Namba 2 kijiji cha Nyaligongo kata ya Mwakitolyo wilaya ya Shinyanga na vitu mbalimbali baada ya kuharibiwa na wananchi wenye hasira kali
Muonekano wa ofisi ya Mwenyekiti wa Kitongoji Namba 2 kijiji cha Nyaligongo kata ya Mwakitolyo wilaya ya Shinyanga na vitu mbalimbali baada ya kuharibiwa na wananchi wenye hasira kali
Muonekano wa pikipiki ya Kamanda wa Sungusungu Buyaga Kazimoto baada ya kuchomwa moto na wananchi wenye hasira kali
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Shinyanga, Ngasa Mboje (katikati) akimweleza jambo Katibu Tawala wilaya ya Shinyanga Boniphace Chambi ( mwenye suti kushoto) wakiwasili katika Kitongoji Namba 2 kijiji cha Nyaligongo kata ya Mwakitolyo wilaya ya Shinyanga kuzungumza na wananchi
Katibu Tawala wilaya ya Shinyanga Boniphace Chambi akizungumza na wananchi wa Kitongoji Namba 2 kijiji cha Nyaligongo kata ya Mwakitolyo wilaya ya Shinyanga
Sehemu ya Wananchi wa Kitongoji Namba 2 kijiji cha Nyaligongo kata ya Mwakitolyo wilaya ya Shinyanga wakimsikiliza Katibu Tawala wilaya ya Shinyanga Boniphace Chambi
Sehemu ya Wananchi wa Kitongoji Namba 2 kijiji cha Nyaligongo kata ya Mwakitolyo wilaya ya Shinyanga wakimsikiliza Katibu Tawala wilaya ya Shinyanga Boniphace Chambi
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP George Kyando akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 19,2022
Na Kadama Malunde – Malunde 1 blog
Wananchi wenye hasira kali wamevunja nyumba na ofisi ya Mwenyekiti wa Kitongoji Namba 2 kijiji cha Nyaligongo kata ya Mwakitolyo wilaya ya Shinyanga Shaban Hamis Zoro kisha kuchoma moto pikipiki na kuvunja nyumba ya Kamanda wa Jeshi la jadi sungusungu Buyaga Kazimoto baada ya mlinzi kudaiwa kuua mchimbaji madini aitwaye Jackson Joseph (35) akigombana mkewe Esther Emmanuel (25).
Inaelezwa kuwa mwanaume aitwaye Jackson Joseph (35) aliuawa Mei 17,2022 majira ya saa tano usiku kwa kupigwa risasi na mlinzi wa Kampuni Binafsi ya Light Ndovu Security aitwaye Abdul Chacha aliyefika nyumbani kwa marehemu akiwa na wenzake watatu pamoja na kamanda wa Sungusungu Buyaga Kazimoto baada ya kupewa taarifa kuwa Jackson Joseph anagombana na mkewe Esther Emmanuel.
Kwa mujibu wa mashuhuda kutoka eneo la tukio, wameieleza Malunde 1 blog kuwa wananchi hao baada ya kupata taarifa ya tukio hilo kesho yake (Mei 18,2022) walichukua maamuzi hayo ya kuvunja ofisi ya mwenyekiti wa kitongoji na nyumba kutokana na kuchoshwa na vitendo vya uonevu ikiwemo Faini kubwa na rushwa vinavyofanywa na makamanda wa Sungusungu huku mwenyekiti wa kitongoji akituhumiwa kufumbia macho vitendo hivyo bila kuchukua hatua wakati makamanda hao wanafanyia kazi zao kwenye ofisi ya afisa mtendaji huyo.
Inadaiwa kuwa wananchi hao walichukizwa na kitendo cha walinzi hao wakiongozwa na kamanda wa Jeshi la sungusungu kusababisha mauaji ya mwananchi huyo kisa anagombana na mke wake huku wakibainisha kuwa wamechoshwa na uonevu kwani badala ya kuwafikisha watuhumiwa kwenye vyombo vya dola wao walinzi hao na kamanda wa sungusungu wamekuwa wakiomba pesa na wasipopewa wanawashambulia watuhumiwa.
Kufuatia tukio hilo, Katibu Tawala wilaya ya Shinyanga Boniphace Chambi kwa niaba ya Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko amefika katika eneo hilo na kuzungumza na wananchi hao huku akivunja uongozi wa kitongoji cha Namba 2 kijiji cha Nyaligongo pamoja na uongozi wa jeshi la sungusungu eneo hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi Mei 19,2022 Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP George Kyando amesema tukio la mauaji limetokea Mei 17,2022 majira ya saa tano usiku katika kitongoji cha Namba 2 kijiji cha Nyaligongo kata ya Mwakitolyo halmashauri ya Shinyanga.
“Jackson Joseph (35) ambaye ni mchimbaji wa madini alikuwa na ugomvi na mkewe, wakati wanaendelea na ugomvi ndipo mkewe akakimbilia nyumba ya jirani,ndipo majirani wakapiga simu kwa kamanda wa jeshi la Sungusungu Buyaga Kazimoto kumtaarifu juu ya ugomvi uliokuwa unaendelea. Ndipo Kamanda huyo wa Sungu alipofika nyumbani kwa Jackson Joseph akiwa na walinzi wanne wa kampuni binafsi, kati yao watatu walikuwa na silaha na mmoja alikuwa na kirungu”, anaeleza Kamanda Kyando.
“……Baada ya Jackson Joseph kuona walinzi wakiwa na silaha ndipo akaanza kukimbia, mlinzi aitwaye Abdul Chacha akiwa na silaha akamkamata Jackson Joseph lakini Jackson akaanza kumnyang’anya mlinzi bunduki ndipo risasi ikafyatuka na kumpiga tumboni na kusababisha kifo chake papo hapo”,anasimulia Kamanda Kyando.
Amesema baada ya wananchi kupata taarifa za kifo cha mwenzo ndipo wakaanza kufuatilia jambo hilo wakajikusanya na kwenda kuchoma moto pikipiki aina ya SUNLG yenye namba za usajili MC BRH ya Kamanda wa Sungusungu Buyaga Kazimoto na kuvunja vunja nyumba yake lakini pia wakavunja nyumba yenye vyumba vitano na duka la mwenyekiti wa kitongoji na ofisi ya mwenyekiti huyo wa kitongoji cha Namba 2 kijiji cha Nyaligongo, Shaban Hamis Zoro.
“Wananchi hao wanadai kuwa mwenyekiti wa Kitongoji anawalea sungusungu ambao wanafanya dhuluma ya kutoza wananchi wanaofanya makosa faini kubwa na rushwa ndani ya ofisi hiyo, anajua maovu yanayofanywa lakini hachukui hatua na wanahoji kwanini walinzi wachukue silaha kwenda kwenye ugomvi wa mtu na mke hadi wasababishe kifo?”,amesema Kamanda Kyando.
Kamanda Kyando amesema tayari wanamshikilia mlinzi wa Kampuni Binafsi ya Light Ndovu Security aitwaye Abdul Chacha kwa tuhuma za mauaji huku wakiendelea kufanya uchunguzi juu ya tukio hilo na kuwatafuta wananchi waliochoma nyumba,pikipiki na ofisi ya mwenyekiti wa kitongoji hicho.
Kamanda Kyando ametoa wito kwa baadhi ya viongozi wanaonyanyasa wananchi kuacha kukandamiza wananchi huku akiwataka walinzi kuwa makini na matumizi ya silaha na kwamba Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga litafanya ukaguzi kwenye makampuni ya ulinzi na kutoa mafunzo ya matumizi ya silaha.
Social Plugin