Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MCHECHU ADAI JPM HAKUMNG’OA NHC, ALALAMIKA KUCHAFULIWA, AFUNGUA KESI, ADAI FIDIA YA BILIONI 3


Na Mwandishi Wetu

MKURUGENZI Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Nehemia Mchechu ameiomba Mahakama iamuru Gazeti la The Citizen kumlipa fidia ya Sh bilioni tatu na kumwomba radhi, kwa madai ya kumchafulia jina na kushusha hadhi na heshima yake katika jamii.

Mchechu ambaye amerejeshwa kwenye nafasi hiyo hivi karibuni na Rais Samia Suluhu Hassan, alitoa madai hayo juzi mbele ya Jaji Leila Mgonya wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Dar es Salaam.


Katika kesi hiyo, Mchechu anatetewa na mawakili Vitalis Peter na Aliko Mwamanenge wakati Gazeti la Citizen linatetewa na mawakili Ambrose Nkwera na Raban Rugina.


Akitoa utetezi wake mahakamani hapo, Mchechu alidai kuwa habari iliyochapishwa na Gazeti hilo na kumhusisha na tuhuma za ubadhirifu na matumizi mabaya ya ofisi, imemshushia hadhi, heshima aliyoijenga kwa zaidi ya miaka 20 ndani na nje ya nchi.


Machi 23 2018, Gazeti la Citizen liliandika habari iliyobeba kichwa cha habari: “Why JPM dissolved NHC Board, Sacked Mchechu (Kwa nini JPM alivunja Bodi ya NHC na kumng’oa Mchechu?).

Habari hiyo iliyoainisha sababu kadhaa wa kadhaa kutoka vyanzo vyake mbalimbali, zinazodaiwa kuwa sababu za Rais wa awamu ya tano, Dk John Magufuli, kuchukua uamuzi wa kuivunja Bodi ya NHC na kumwondosha Mkurugenzi Mkuu, Mchechu.

Madai

Baadhi ya tuhuma zalizoibuliwa kwenye habari hiyo, ni pamoja na madai kwamba Mchechu alikuwa akichunguzwa na Bodi ya Wakurugenzi ya NHC na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuhusu mgongano wa madaraka juu ya ununuzi wa ekari 500 za mradi wa NHC Safari City, Arusha.

Pia Gazeti hilo lilidai kuwa Mchechu anachunguzwa na TAKUKURU kwa madai ya kumtumia mkandarasi aliyekodishwa na NHC, kujenga barabara yake binafsi karibu na mradi huo wa NHC Safari City.

Kuhusu mradi wa Kawe, Gazeti hilo lilidai kuwa Mchechu aliingia makubaliano na kampuni ya ukandarasi ya PHILS International yenye makao yake Dubai, bila kushirikisha kitengo cha ununuzi wa NHC, kinachoongozwa na Hamis Mpinda.



Hoja zingine zilizotajwa kwenye habari hiyo, ni kuhusu madai kwamba Mchechu anachunguzwa kwa tuhuma kuwa kampuni ya mkewe, ilipewa zabuni ya kutoa huduma za bima kwenye nyumba za NHC Mtwara, hali ambayo ni kinyume na maadili ya utumishi wa umma.

Madai ya mwisho yaliyotajwa na gazeti hilo ni tuhuma za matumizi mabaya ya ofisi yaliyotajwa kwa kiwango kikubwa.

Utetezi wake

Akitoa utetezi wake juzi mahakamani hapo, Mchechu alidai kuwa habari hiyo ilikuwa ya uongo na yenye lengo la kumchafulia jina na kumvunjia heshima, kwani wahusika hawakumhoji ili kuthibitisha madai hayo.

Huku akiongozwa na Wakili Vitalis, Mchechu alidai kuwa Gazeti hilo liliandika habari hiyo, kuwa ameng’olewa kwenye nafasi yake na Rais Magufuli, huku likijua fika kuwa hakung’olewa na Rais.

Akifafanua hoja hiyo, Mchechu alidai kuwa alipewa likizo na hata wakati Gazeti hilo linachapishwa, alikuwa bado mfanyakazi wa Shirika hilo.

“Mheshimiwa Jaji, Gazeti hili liliniandika vibaya, kwanza kwenye kichwa chake cha habari ukurasa wa mbele kwa maandishi makubwa na yaliyokaziwa kuwa, “Why JPM dissolved NHC Board, Sacked Mchechu”.


“Mheshimiwa Jaji, liliandika habari hii likijua kuwa sijafukuzwa, kwa kuwa nilikuwa sijafukuzwa kazi na wala Mheshimiwa Rais hakuwa na hakuwahi kunifukuza kazi.

“Kwa hiyo hii ilikuwa ni habari ya uongo na yenye nia ovu ya kunichafua na kunishushia hadhi yangu katika familia, jamii, Taifa na duniani kwa ujumla,” alidai Mchechu.

Kuhusu madai kuwa alihojiwa na TAKUKURU, Mchechu alidai hakuwahi kuhojiwa na chombo hicho wala chombo kingine chochote juu ya mgongano wa ununuzi wa ekari 500 za NHC kwa ajili ya mradi wa NHC Safari City.

Katika tuhuma hiyo, Mchechu anadaiwa kuwa ndiye aliyewauzia NHC kiwanja hicho kwa bei kubwa zaidi kuliko bei halisi.

Akitoa utetezi wake katika hilo, Mchechu alidai kuwa kwanza NHC haijawahi kununua ekari 500 Arusha na ukweli halisi ni kuwa NHC ilinunua ekari 583.

“Binafsi sikuwahi kuhojiwa wala kuchunguzwa, iwe na Bodi au taasisi yoyote ya uchunguzi, ikiwamo TAKUKURU juu ya ununuzi wa shamba la ekari 500 au lolote Arusha,” alidai Mchechu.

Mlalamikaji huyo alidai kuwa hajawahi kumiliki au kununua ardhi Arusha katika maisha yake yote, na hata katika kampuni anazomiliki, hazijawahi kumiliki au kununua ardhi Arusha.


“Na sijawahi kuiuzia NHC ardhi Arusha na pia mahali pengine popote Tanzania, kabla sijawa mtumishi au nilipokuwa mtumishi katika uhai wa maisha yangu yote mpaka leo,” alidai Mchechu.

Kuhusu madai kuwa anachunguzwa kwa kumtumia mkandarasi wa NHC kwa mradi wake binafsi, Mchechu alidai kuwa hajawahi kutumia mkandarasi yeyote wa NHC, hata asiye wa NHC kuandaa barabara katika ardhi yake binafsi, inayotajwa kuwa karibu na mradi wa Safari City kwa kutumia fedha za Shirika hilo.

“Na pia tofauti na tuhuma hii, ukweli ni kuwa sina na sijawahi kuwa na ardhi karibu na mradi wa NHC Safari City na hata mkoa mzima wa Arusha katika maisha yangu yote,” alisisitiza.

Kuhusu mradi wa Kawe, Mchechu alidai kuwa hajawahi kukiuka taratibu za sheria ya ununuzi kuhusu mradi huo.


“Kama ilivyo sheria ya ununuzi wa umma, uamuzi wa zabuni ya mradi wa Kawe, huamuliwa na Bodi ya Zabuni ya Shirika. Sijawahi kukiuka taratibu za sheria ya ununuzi kwa kufanya au kupoka uamuzi wa Bodi ya Zabuni kwa mradi wa Kawe, au mradi wowote ambao Shirika lilifanya.

“Kwa maana hiyo, sikuwa na wajibu wa kumshirikisha aliyekuwa Mkuu wa Kitengo cha Ununuzi cha NHC, Hamisi Mpinda kwa jambo ambalo halikuwa katika uamuzi wangu,” alidai.


Madai kuhusu kutumia kampuni ya mkewe, kutoa huduma ya bima kwa nyumba za NHC Mtwara, Mchechu alidai kuwa Shirika halikati bima kwa majengo yake, bali hutumia mfuko maalumu wa pesa (Sinking Fund) kwa ajili ya bima ya majengo yake, hivyo kampuni ya mkewe haijawahi kutoa huduma ya bima kwa NHC.

Akijibu madai ya matumizi mabaya ya ofisi, Mchechu alidai hajawahi kuchunguzwa au kuitwa kuhojiwa na kamati yoyote, juu ya ukosefu wa maadili na matumizi mabaya wa fedha za umma.

“Na hakujawahi kuwa na taarifa ya uchunguzi iliyonitia hatiani kwa matumizi mabaya ya fedha za umma na ukosefu wa maadili,” alidai.

Athari

Mchechu alidai kuwa taarifa hiyo imemwathiri kwenye maeneo mengi katika maisha yake, kwani iliwafikia watu wengi ndani na nje ya nchi.

Alidai kuwa habari hiyo ilimsababishia mfadhaiko mkubwa wa akili, msongo wa mawazo, hofu na kudhuru afya yake.

“Nilikosa kuaminika, na hivyo kupoteza nafasi nyingi za kibiashara nilizokuwa nafanya na wenzangu wa kibiashara, na kuondokewa na baadhi ya wabia katika kampuni ambazo nina uhusiano nazo kibiashara.

“Taarifa hii iliathiri hata kuaminika kwa taasisi niliyokuwa naiongoza na hivyo kuathiri ufanisi na utendaji wake wa kazi, na kuaminika kwake kwa wateja,” alisema.

Mbali na kuwa Mkurugenzi wa NHC, Mchechu kwa sasa pia ni Mwenyekiti wa Benki ya BOA, Mwenyekiti wa Kampuni za Amboni Group of Companies, Amboni Beach Properties na Amboni Sisal Limited.

Pia Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa TANESCO, TANTRADE, TMRC, Kampuni ya Watumisihi Housing, mjumbe wa Bodi ya Chuo Kikuu cha Tumaini tawi la Dar es Salaam, Katibu wa Usharika wa Kanisa la KKKT Usharika wa Mbezi Beach na pia Mwenyekiti wa Halmashauri ya Fedha na Mipango wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani (DMP) kama sehemu tu ya majukumu yake.

Kesi hiyo itaendelea kusikilizwa Mei 20 mwaka huu ambapo mawakili wa utetezi wataanza kumhoji.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com