Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

UTEKELEZAJI MKATABA WA SOKO LA ENEO HURU LA KIBIASHARA AFRIKA KUKUZA FURSA ZA BIASHARA



Na Rahma Idrisa - Zanzibar
Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Mhe.  Omar Said Shaaban amesema utekelezaji wa mkataba wa soko la eneo huru la kibiashara Afrika utasaidia kukuza fursa za kibiashara katika kuhakikisha wanafikia malengo ya kuwa na soko la pamoja.


Akifungua warsha ya siku moja kwa Wabunge na Wawakilishi kuhusu mkataba wa eneo huru la biashara Afrika iliyofanyika katika ukumbi wa hoteli ya Sea Cliff iliyopo Bubwini mkoa wa Kaskazin B.


Amesema lengo kuu la warsha hiyo ni kutoa uelewa kwa watendaji hao ili kuona wanatambua fursa zilizopo ikiwemo za biashara na uwekezaji nchini.


"Mkataba huu unaenda kutoa fursa za kufanya biashara ya pamoja hivyo utasaidia sana kuweka mazingira yaliyo bora katika kutanua biashara zilizomo ndani ya nchi za Afrika na kuzitangaza duniani kote",  amesema Shaaban


Amesema Tanzania kisheria ni wajumbe halali wa mkataba huo ambapo imechangia kwa kiasi kikubwa kuwepo kwa mkataba huo kwa kuamini kuwa itasaidia kuimarisha masuala ya kiuchumi kwa ajili ya nchi.


Waziri Shaabani ameongezea kuwa serikali imeshafanya utafiti wa kina juu ya mkataba huo unaohusisha zaidi ya nchi 50 ili kuona unakuwa shirikishi ikiwemo mpango wa nchi ndogo za visiwa hasa katika kufanikiwa ,kuzalisha na kuingiza sokoni bidhaa zinazozalishwa nchini ikiwemo viungo.


"Kwa sasa serikali inajikita zaidi katika kuhakikisha wanaendelea kutoa elimu kuhusu mkataba huo kwa wadau wa masuala mbalimbali ya biashara ili kuona unatambulika na hatimaye kutoa matunda kama ilivyotarajiwa ikiwemo namna ya kuzalisha na kutengeneza vifungashio vyenye ubora unaokubalika", amesema.


Aidha ameishukuru benki ya Afrexim kwa kutekeleza mkataba huo .


Naye mwakilishi wa benki ya Afrexim Dkt. Emeka Ozomba amesema kuwa kuwepo kwa mifumo bora ya kibiashara na uchumi kutasaidia kwa kiasi kikubwa wananchi wa bara la Afrika wapatao bilioni 1.3 kupata ajira kupitia biashara ya soko hilo.


"Tunapoboresha mifumo ya biashara na kuweka mifumo iliyokuwa bora ni lazima watu wengi watanufaika na ajira ikiwemo vijana kwani kila siku zinavyokwenda mifumo ya ufanyaji kazi huwa inabadilika badilika katika nchi zetu",amesema.


Mtendaji Mkuu wa Sekretarieti ya mkataba wa eneo huria la biashara Afrika EFCFTA Wamkele Mene amesema lengo kuu ni kuona wanatafuta njia bora katika kuimarisha masuala ya kibiashara kati ya umoja huo wa Afrika.

Kwa upande wake Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Umwagiliaji kutoka Zanzibar Shamata Shaame Khamis amesema kuwa bidhaa nyingi zinazozalishwa Zanzibar zimekuwa zinakosa soko la uhakika jambo linalopelekea bidhaa kupotea ,hivyo mkataba huo utaleta fursa kubwa kwa wafanya biashara katika maeneo mbalimbali.


"Tunaona kuwa wakulima wengi wa tungule, ndizi, embe, nanasi , na matunda mengine wamekuwa wakikosa soko la uhakika mara kwa mara jambo linalopelekea bidhaa nyingi kuharibika na kuingia katika hasara", amesema.


Baadhi ya washiriki wa warsha hiyo akiwemo Yussuf Hassan Idi mwenyekiti kamati ya kilimo biashara na utalii kutoka baraza la wawakilishi wameshauri umuhimu wa wajasiri amali kuzalisha bidhaa zenye ubora kwani kutakuwa na ushindani mkubwa wa bidhaa zitakazouzwa kupitia soko hilo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com