HILI NDIYO JIJI LA STAREHE DUNIANI, LINAELEA BAHARINI, BATA MWANZO MWISHO



Bila shaka sote tunazijua meli, iwe ni kwa kuiona live au kwenye picha, au kwa kupanda kabisa! Meli ni chombo cha usafiri majini chenye uwezo wa kubeba abiria na mizigo. Zipo meli kibao, kubwa na ndogo lakini ukiwauliza wengi meli kubwa zaidi waliyowahi kuiona au kusikia habari zake, basi watakutajia Meli ya Titanic.
Achana na stori zote hizo, je, umewahi kuona mji unaotembea baharini? Yaani namaanisha hivi, umewahi kuona ‘bonge’ la meli ambayo ndani yake kuna huduma zote muhimu zinazopatikana kwenye miji mikubwa duniani huku ikiwa imebeba idadi kubwa ya watu wanaotosha kuujaza mji mzima?


Kama bado, basi nakujuza kwamba Allure of The Sea ni meli kubwa zaidi kuliko zote za abiria kwa sasa, ikiwa imebandikwa jina la Jiji Linalotembea Baharini kutokana na ukubwa wake pamoja na vitu vilivyomo ndani yake.
Ukianza na suala la ukubwa wa meli hii inayomilikiwa na Kampuni ya Royal Caribbean International, ina urefu wa mita 360 na uzito wa tani 54,000, ikiwa na uwezo wa kubeba abiria 6,400, mizigo yenye uzito wa tani 225,282 na zaidi ya wahudumu 2100.


Meli hiyo imetengenezwa na Kampuni ya STX Europe yenye makao makuu yake, Turku nchini Finland na ujenzi wake ulikamilika November 2009, ambapo kwa zaidi ya miaka nane imekuwa ikiendelea kuboreshwa mazingira yake ya ndani ili kuendana na mahitaji ya abiria na tayari meli hiyo imeshaanza safari zake.


Thamani ya meli nzima, ni dola za Kimarekani 1.13 bilioni, ambazo ni sawa na …. na meli hiyo imetengenezwa mahususi kwa ajili ya wapenda burudani na ‘kula bata’.


Miongoni mwa vivutio vilivyopo ndani ya meli hiyo ni pamoja na ukumbi wa muziki wa ghorofa mbili, ukumbi wa sinema wenye viti 1380, uwanja wa kuteleza kwenye barafu (ice skating) na mahoteli makubwa 25 yakiwa na vyakula vya aina tofautitofauti.



Kuna jumla ya mabwawa 21 ya kuogelea, baa zipatazo 40 zinazouza pombe aina mbalimbali kutoka maeneo tofauti duniani, kiwanja cha mpira wa kikapu, kiwanja cha gofu, gym, massage parlour, barbershops na huduma nyingine kibao.



Ndani ya meli hiyo, kuna kumbi za sinema ambazo uongozi wa kampuni inayomiliki meli hiyo, umeingia mkataba na Kampuni ya DreamWorks ya Marekani, ambapo filamu mpya za Hollywood huwa zinazinduliwa ndani ya meli hiyo karibu kila mwisho wa wiki huku pia mastaa kibao waliopo chini ya kampuni hiyo, wakijumuika na mashabiki wao ndani ya meli.



Kuna burudani nyingine kibao ndani ya meli hiyo, ‘live band’ kama zote huku wasanii kutoka kwenye lebo mbili kubwa za muziki za Broadway na West End wakiwa na kazi moja tu, ya kuwaburudisha wasafiri ndani ya meli hiyo.
Pia kuna kundi maalum la sarakasi liitwalo The Blue Planet ambalo kila jioni hufanya maonesho maalum ndani ya kumbi za burudani kwenye meli hiyo.



Pia ndani ya meli hiyo, kuna ukumbi wa maonesho ya sanaa (art gallery) za nchi mbalimbali, kuna supermarket kubwa yenye ghorofa mbili na ‘vikorombwezo’ vingine kibao.



Abiria wanaoingia kwenye meli hiyo, ambao kama nilivyosema ni 6,400, wanatajwa kuwa ni wengi kuliko idadi ya watu waliopo kwenye miji mbalimbali nchini Australia. Meli hiyo imekuwa ikipiga ruti kuelekea miji mbalimbali, ikitokea kwenye Bandari ya Lauderdale, Florida nchini Marekani ambako ndiko ‘nyumbani’ kwake.



Maeneo ambayo meli hiyo huenda ni pamoja na Mexico, Jamaica and Visiwa vya Bahamas huku nauli ya chini kabisa ikiwa ni dola za Kimarekani 1,149. Kampuni ya Royal Carribean, inafikiria kuongeza safari za meli hiyo, ili iwe inafika mpaka barani Afrika na kwingineko, na kuongeza uhuru wa watu kula bata!



Pia kampuni iliyotengeneza meli hiyo, imeeleza kwamba ina mpango wa kutengeneza meli nyingi zaidi za aina hiyo, baada ya mafanikio makubwa yaliyopatikana tangu kuzinduliwa kwa Allure of The Sea, kwa hiyo si ajabu miaka michache baadaye ngoma ikatia nanga pale Bandari ya Dar es Salaam kwa ajili ya watu kwenda kula bata.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post