Waziri wa katiba na sheria Dkt. Damas Ndumbaro (katikati) akizungumza kwenye mkutano wa Chama Cha Mawakili Tanzania TLS unaofanyika jijini Arusha.
Na Rose Jackson,Arusha
Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Damas Ndumbaro ametoa siku 30 kwa Mawakili wote kuhakikisha wanakuwa na mihuri ya kielektoniki.
Dkt. Ndumbaro Ameyasema hayo wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Chama Cha mawakili Tanzania (TLS) unaofanyika jijini Arusha.
Amesema kuwa ndani ya siku 30 mawakili wote lazima wawe na mihuri ya kielektoniki na baada ya hapo hawatatambua mihuri ambayo sio ya kielektoniki.
Ameongeza kuwa kwa miaka mingi kumekuwa na malalamiko ya watu kujifanya mawakili na kutumia mihuri ya mawakili hivyo anaamini kupitia mihuri ya kielektoniki ambayo imeandaliwa na TLS ambayo ameizindua anaamini itamaliza changamoto hiyo.
"Ndani ya siku 30 lazima mawakili wawe na mihuri na tutaandikia mamlaka zote zinazotambua mihuri ya mawakili maelekezo ikiwemo TRA juu ya kuhakikisha mawakili wote wanakuwa na mihuri hii ya kielektoniki lengo ni kuondoa malalamiko ya watu wanaotumia mihuri ya mawakili", ameongeza Dkt. Ndumbaro.
Kwa upande wake Rais wa chama Cha mawakili Tanzania Dr Edward Hosea amesema kuwa mkutano huo umekutanisha mawakili wote kutoka Tanzania ambao ni wanachama.
Amesema kutakuwa na mada tofauti zitakasowakilishwa na mawakili na kwamba wamekuwa wakifanya kazi zao kwa kushirikiana na serikali ili waweze kutimiza majukumu yao kama nchi.
Amesema wamekuwa wakifanya mkutano huo kila mwaka na wanatarajia kujadili mada ambazo zitaleta tija na ufanisi katika chama hicho.
Hata hivyo katika mkutano huo Waziri Ndumbaro amezindua mihuri ya kielektoniki na kuzindua Saccos ya mawakili.