Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WATUHUMIWA UBADHILIFU FEDHA KUKATWA ASILIMIA 15 CHATO

 

Na Daniel Limbe, Chato

WATUMISHI wanne kati ya tano waliokuwa wakikabiliwa na tuhuma za ubadhilifu wa fedha kwenye halmashauri ya wilaya ya Chato mkoani Geita, imeazimiwa kukatwa asilimia 15 ya mishahara yao.

Fedha hizo zitakatwa kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo ikiwa ni adhabu kwa makosa waliyotenda kabla ya kisimamishwa kazi mwaka jana.

Uamuzi huo umetolewa na mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo, Christian Manunga, muda mfupi baada ya Baraza la madiwani hao kujigeuza kamati kwa lengo la kujadili hoja ya watumishi hao.

"Baada ya majadiliano yetu kukamilika tumekubaliana kwa pamoja kuwa watumishi watano wa idara ya ugavi tuliowasimamisha kazi mwaka jana kwa tuhuma za ubadhilifu wa fedha wasamehewe na walejeshwe kazini",alisema.

"Hata hivyo uchunguzi wetu ulibaini mtumishi mmoja kati yao hakuna sehemu yoyote aliyoonekana kusaini nyaraka ispokuwa ni mlevi...kwahiyo wenzake wanne watakatwa aslimia 15 ya mishahara yao kwa kipindi cha miaka mitatu",alisema Manunga.

Kaimu mkurugenzi wa halmashauri hiyo,Ismael Mgoba,alisisitiza kuwa uamuzi huo umetolewa kwa mujibu wa kanuni za utumishi wa Umma, huku akidai hatua hiyo ni fundisho kwa watumishi wengine wenye nia ya kutenda kosa kama hilo.

"Uamuzi huu umezingatia sheria, taratibu na kanuni za utumishi wa Umma...hii ni adhabu moja wapo kati ya zingine zilizoainishwa iwapo mtumishi atathibitika kufanya makosa kama hayo",alisema.

Amewataka watumishi kufanya kazi kwa weledi wa hali ya juu pamoja na kutanguliza maslahi ya jamii mbele badala ya maslahi binafsi kwa madai hali hiyo inaweza kusababisha kupoteza ajira zao.

Wakati uamuzi huo ukitolewa mkuu wa wilaya ya Chato, Martha Mkupasi, alikuwa kando akisikiliza kwa kina.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com